0:00
0:00

Mlango 83

Ee Mungu, usistarehe, Ee Mungu, usinyamae, wala usitulie.
2 Maana adui zako wanafanya ghasia, Nao wakuchukiao wameviinua vichwa vyao.
3 Juu ya watu wako wanafanya hila, Na kushauriana juu yao uliowaficha.
4 Wamesema, Njoni, tuwakatilie mbali wasiwe taifa, Na jina la Israeli halitakumbukwa tena.
5 Maana wanashauriana kwa moyo mmoja, Juu yako wanafanyana agano.
6 Hema za Edomu, na Waishmaeli, Na Moabu, na Wahagari,
7 Gebali, na Amoni, na Amaleki, Na Filisti, nao wanaokaa Tiro,
8 Ashuri naye amepatana nao, Wamewasaidia wana wa Lutu.
9 Uwatende kama Midiani, kama Sisera, Kama Yabini, penye kijito Kishoni.
10 Ambao waliangamizwa Endori; Wakawa samadi juu ya nchi.
11 Uwafanye wakuu wao kama Orebu na Zeebu, Na masheki yao wote kama Zeba na Zalmuna.
12 Ambao Walisema, Na tutamalaki makao ya Mungu.
13 Ee Mungu, uwafanye kama mavumbi ya kisulisuli, Mithili ya makapi mbele ya upepo,
14 Kama moto uteketezao msitu, Kama miali ya moto iiwashayo milima,
15 Ndivyo utakavyowafuatia kwa tufani yako, Na kuwafadhaisha kwa dhoruba yako.
16 Uwajaze nyuso zao fedheha; Wakalitafute jina lako, Bwana.
17 Waaibike, wafadhaike milele, Naam, watahayarike na kupotea.
18 Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote.