0:00
0:00

Mlango 33

Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
2 Mshukuruni Bwana kwa kinubi, Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
3 Mwimbieni wimbo mpya, Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.
4 Kwa kuwa neno la Bwana lina adili, Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
5 Huzipenda haki na hukumu, Nchi imejaa fadhili za Bwana.
6 Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.
7 Hukusanya maji ya bahari chungu chungu, Huviweka vilindi katika ghala.
8 Nchi yote na imwogope Bwana, Wote wakaao duniani na wamche.
9 Maana Yeye alisema, ikawa; Na Yeye aliamuru, ikasimama.
10 Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa, Huyatangua makusudi ya watu.
11 Shauri la Bwana lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.
12 Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao, Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
13 Toka mbinguni Bwana huchungulia, Huwatazama wanadamu wote pia.
14 Toka mahali pake aketipo Huwaangalia wote wakaao duniani.
15 yeye aiumbaye mioyo yao wote Huzifikiri kazi zao zote.
16 Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu.
17 Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake.
18 Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake.
19 Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa.
20 Nafsi zetu zinamngoja Bwana; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
21 Maana mioyo yetu itamfurahia, Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takatifu.
22 Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, Kama vile tulivyokungoja Wewe.