0:00
0:00

Mlango 2

Mbona mataifa wanafanya ghasia, Na makabila wanatafakari ubatili?
2 Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya shauri pamoja, Juu ya Bwana, Na juu ya masihi wake.
3 Na tuvipasue vifungo vyao, Na kuzitupia mbali nasi kamba zao.
4 Yeye aketiye mbinguni anacheka, Bwana anawafanyia dhihaka.
5 Ndipo atakaposema nao kwa hasira yake, Na kuwafadhaisha kwa ghadhabu yake.
6 Nami nimemweka mfalme wangu Juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu.
7 Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.
8 Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, Na miisho ya dunia kuwa milki yako.
9 Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi.
10 Na sasa, enyi wafalme, fanyeni akili, Enyi waamuzi wa dunia, mwadibiwe.
11 Mtumikieni Bwana kwa kicho, Shangilieni kwa kutetemeka.
12 Shikeni yaliyo bora asije akafanya hasira, Nanyi mkapotea njiani,Kwa kuwa hasira yake itawaka upesi,Heri wote wanaomkimbilia.