0:00
0:00

Mlango 81

Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha, Mshangilieni Mungu wa Yakobo.
2 Pazeni zaburi, pigeni matari, Kinubi chenye sauti nzuri, na kinanda.
3 Pigeni panda mwandamo wa mwezi, Wakati wa mbalamwezi, sikukuu yetu.
4 Kwa maana ni sheria kwa Israeli, Ni hukumu ya Mungu wa Yakobo.
5 Aliamuru iwe ushuhuda katika Yusufu, Alipoondoka juu ya nchi ya Misri; Maneno yake nisiyemjua naliyasikia.
6 Nimelitenga bega lake na mzigo, Mikono yake ikaachana na kikapu.
7 Katika shida uliniita nikakuokoa; Nalikuitikia katika sitara ya radi; Nalikujaribu penye maji ya Meriba.
8 Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya, Ee Israeli, kama ukitaka kunisikiliza;
9 Usiwe na mungu mgeni ndani yako; Wala usimsujudie mungu mwingine.
10 Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, Niliyekupandisha toka nchi ya Misri; Fumbua sana kinywa chako nami nitakijaza.
11 Lakini watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu, Wala Israeli hawakunitaka.
12 Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao, Waenende katika mashauri yao.
13 Laiti watu wangu wangenisikiliza, Na Israeli angeenenda katika njia zangu;
14 Ningewadhili adui zao kwa upesi, Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu;
15 Wamchukiao Bwana wangenyenyekea mbele zake, Bali wakati wao ungedumu milele.
16 Naam, ningewalisha kwa unono wa ngano, Ningewashibisha kwa asali itokayo mwambani.