0:00
0:00

Mlango 80

Wewe uchungaye Israeli, usikie, Wewe umwongozaye Yusufu kama kundi; Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.
2 Mbele ya Efraimu, na Benyamini, na Manase, Uziamshe nguvu zako, Uje, utuokoe.
3 Ee Mungu, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.
4 Ee Bwana, Mungu wa majeshi, hata lini Utayaghadhibikia maombi ya watu wako?
5 Umewalisha mkate wa machozi, Umewanywesha machozi kwa kipimo kikuu.
6 Unatufanya sababu ya ugomvi kwa jirani zetu, Na adui zetu wanacheka wao kwa wao.
7 Ee Mungu wa majeshi, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.
8 Ulileta mzabibu kutoka Misri, Ukawafukuza mataifa ukaupanda.
9 Ulitengeneza nafasi mbele yake, Nao ukatia mizizi sana ukaijaza nchi.
10 Milima ilifunikwa kwa uvuli wake, Matawi yake ni kama mierezi ya Mungu.
11 Nao uliyaeneza matawi yake hata baharini, Na vichipukizi vyake hata kunako Mto.
12 Kwa nini umezibomoa kuta zake, Wakauchuma wote wapitao njiani?
13 Nguruwe wa msituni wanauharibu, Na hayawani wa kondeni wanautafuna.
14 Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi, Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu.
15 Na mche ule ulioupanda Kwa mkono wako wa kuume; Na tawi lile ulilolifanya Kuwa imara kwa nafsi yako.
16 Umechomwa moto; umekatwa; Kwa lawama ya uso wako wanapotea.
17 Mkono wako na uwe juu yake Mtu wa mkono wako wa kuume; Juu ya mwanadamu uliyemfanya Kuwa imara kwa nafsi yako;
18 Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma; Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako.
19 Ee Bwana, Mungu wa majeshi, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.