0:00
0:00

Mlango 135

Haleluya. Lisifuni jina la Bwana, Enyi watumishi wa Bwana, sifuni.
2 Ninyi msimamao nyumbani mwa Bwana, Nyuani mwa nyumba ya Mungu wenu.
3 Msifuni Bwana kwa kuwa Bwana ni mwema, Liimbieni jina lake kwa maana lapendeza.
4 Kwa sababu Bwana amejichagulia Yakobo, Na Israeli, wawe watu wake hasa.
5 Maana najua mimi ya kuwa Bwana ni mkuu, Na Bwana wetu yu juu ya miungu yote.
6 Bwana amefanya kila lililompendeza, Katika mbingu na katika nchi, Katika bahari na katika vilindi vyote.
7 Ndiye apandishaye mvuke toka miisho ya nchi; Huifanyia mvua umeme; Hutoa upepo katika hazina zake.
8 Aliwapiga wazaliwa wa kwanza wa Misri, Wa wanadamu na wa wanyama.
9 Alipeleka ishara na maajabu kati yako, Ee Misri, Juu ya Farao na watumishi wake wote.
10 Aliwapiga mataifa mengi, Akawaua wafalme wenye nguvu;
11 Sihoni, mfalme wa Waamori, Na Ogu, mfalme wa Bashani, Na falme zote za Kanaani.
12 Akaitoa nchi yao iwe urithi, Urithi wa Israeli watu wake.
13 Ee Bwana, jina lako ni la milele, Bwana, kumbukumbu lako vizazi hata vizazi.
14 Kwa kuwa Bwana atawaamua watu wake, Atawahurumia watumishi wake.
15 Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu.
16 Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni,
17 Zina masikio lakini hazisikii, Wala hamna pumzi vinywani mwake.
18 Wazifanyao watafanana nazo, Na kila mmoja anayezitumainia.
19 Enyi mlango wa Israeli, mhimidini Bwana; Enyi mlango wa Haruni, mhimidini Bwana;
20 Enyi mlango wa Lawi, mhimidini Bwana; Ninyi mnaomcha Bwana, mhimidini Bwana.
21 Na ahimidiwe Bwana toka Sayuni, Akaaye Yerusalemu. Haleluya.