0:00
0:00

Mlango 74

Ee Mungu, mbona umetutupa milele? Kwa nini hasira yako inatoka moshi Juu ya kondoo wa malisho yako?
2 Ulikumbuke kusanyiko lako, Ulilolinunua zamani. Ulilolikomboa liwe kabila ya urithi wako, Mlima Sayuni ulioufanya maskani yako.
3 Upainulie miguu yako palipoharibika milele; Adui ameufanya kila ubaya katika patakatifu.
4 Watesi wako wamenguruma kati ya kusanyiko lako; Wameweka bendera zao ziwe alama.
5 Wanaonekana kama watu wainuao mashoka, Waikate miti ya msituni.
6 Na sasa nakishi yake yote pia Wanaivunja-vunja kwa mashoka na nyundo.
7 Wamepatia moto patakatifu pako; Wamelinajisi kao la jina lako hata chini.
8 Walisema mioyoni mwao, Na tuwaangamize kabisa; Mahali penye mikutano ya Mungu Wamepachoma moto katika nchi pia.
9 Hatuzioni ishara zetu, wala sasa hakuna nabii, Wala kwetu hakuna ajuaye, hata lini?
10 Ee Mungu, mtesi atalaumu hata lini? Adui alidharau jina lako hata milele?
11 Mbona unaurudisha mkono wako, Naam, mkono wako wa kuume, Uutoe kifuani mwako, Ukawaangamize kabisa.
12 Lakini Mungu ni mfalme wangu tokea zamani, Afanyaye mambo ya wokovu katikati ya nchi.
13 Wewe umeipasua bahari kwa nguvu zako, Umevivunja vichwa vya nyangumi juu ya maji.
14 Wewe uliviseta vichwa vya lewiathani, Awe chakula cha watu wa jangwani.
15 Wewe ulitokeza chemchemi na kijito; Wewe ulikausha mito yenye maji sikuzote.
16 Mchana ni wako, usiku nao ni wako, Ndiwe uliyeufanya mwanga na jua.
17 Wewe uliiweka mipaka yote ya dunia, Kaskazi na kusi Wewe ulizitengeneza.
18 Ee Bwana, uyakumbuke hayo, adui amelaumu, Na watu wapumbavu wamelidharau jina lako.
19 Usimpe mnyama mkali nafsi ya hua wako; Usiusahau milele uhai wa watu wako walioonewa.
20 Ulitafakari agano; Maana mahali penye giza katika nchi Pamejaa makao ya ukatili.
21 Aliyeonewa asirejee ametiwa haya, Mnyonge na mhitaji na walisifu jina lako.
22 Ee Mungu, usimame, ujitetee mwenyewe, Ukumbuke unavyotukanwa na mpumbavu mchana kutwa.
23 Usiisahau sauti ya watesi wako, Ghasia yao wanaokuondokea inapaa daima.