0:00
0:00

Mlango 144

Na ahimidiwe Bwana, mwamba wangu, Anifundishaye mikono yangu vita, Vidole vyangu kupigana.
2 Mhisani wangu na boma langu, Ngome yangu na mwokozi wangu, Ngao yangu niliyemkimbilia, Huwatiisha watu wangu chini yangu.
3 Ee Bwana, mtu ni kitu gani hata umjue? Na binadamu hata umwangalie?
4 Binadamu amefanana na ubatili, Siku zake ni kama kivuli kipitacho.
5 Bwana, uziinamishe mbingu zako, ushuke, Uiguse milima nayo itatoka moshi.
6 Utupe umeme, uwatawanye, Uipige mishale yako, uwafadhaishe.
7 Uinyoshe mikono yako toka juu, uniponye, Unitoe katika maji mengi, katika mkono wa wageni.
8 Vinywa vyao vyasema visivyofaa, Na mkono wao wa kuume ni mkono wa uongo.
9 Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya, Kwa kinanda chenye nyuzi kumi nitakuimbia.
10 Awapaye wafalme wokovu, Amwokoa Daudi, mtumishi wake, na upanga wa uovu.
11 Uniponye, unitoe, Katika mkono wa wageni. Vinywa vyao vyasema visivyofaa, Na mkono wao wa kuume ni mkono wa uongo.
12 Wana wetu na wawe kama miche Waliokua ujanani. Binti zetu kama nguzo za pembeni Zilizonakishwa kwa kupamba hekalu.
13 Ghala zetu na zijae Zenye akiba za jinsi zote. Kondoo zetu na wazae Elfu na makumi elfu mashambani mwetu.
14 Ng'ombe zetu na wachukue mizigo, Kusiwe na kushambuliwa. Wala kusiwe na kuhamishwa, Wala malalamiko katika njia zetu.
15 Heri watu wenye hali hiyo, Heri watu wenye Bwana kuwa Mungu wao.