0:00
0:00

Mlango 141

Ee Bwana, nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo.
2 Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.
3 Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.
4 Usiuelekeze moyo wangu kunako jambo baya, Nisiyazoelee matendo yasiyofaa, Pamoja na watu watendao maovu; Wala nisile vyakula vyao vya anasa.
5 Mwenye haki na anipige, itakuwa fadhili; Anikemee, itakuwa kama mafuta kichwani; Kichwa changu kisikatae, Maana siachi kusali kati ya mabaya yao.
6 Makadhi wao wakiangushwa kando ya genge, Watayasikia maneno yangu, maana ni matamu.
7 Kama kupasua kuni na kuzichanja juu ya nchi, Ndivyo ilivyo mifupa yetu mdomoni pa kuzimu.
8 Macho yangu yanakuelekea Wewe, MUNGU Bwana, Nimekukimbilia Wewe, usiniache nafsi yangu.
9 Unilinde na mtego walionitegea, Na matanzi yao watendao maovu.
10 Wabaya na waanguke katika nyavu zao wenyewe, Pindi mimi ninapopita salama.