0:00
0:00

Mlango 124

Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi, Israeli na aseme sasa,
2 Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi, Wanadamu walipotushambulia.
3 Papo hapo wangalitumeza hai, Hasira yao ilipowaka juu yetu
4 Papo hapo maji yangalitugharikisha, Mto ungalipita juu ya roho zetu;
5 Papo hapo yangalipita juu ya nafsi zetu Maji yafurikayo.
6 Na ahimidiwe Bwana; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao.
7 Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka.
8 Msaada wetu u katika jina la Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.