Ezekieli
Mlango 47
Baadaye akanileta tena mpaka lango la nyumba; na tazama, maji yalitoka chini ya
kizingiti cha nyumba, kwa njia ya mashariki, maana upande wa mbele wa nyumba ulielekea
upande wa mashariki; nayo maji yakashuka toka chini ya upande wa kuume wa nyumba,
upande wa kusini wa madhabahu.
2 Ndipo akanileta nje kwa njia ya lango upande wa kaskazini, akanizungusha kwa njia
ya nje mpaka lango la nje, kwa njia yake iliyoelekea mashariki; na tazama, maji
yalitoka upande wa kuume.
3 Na alipotoka mtu yule, mwenye uzi wa kupimia mkononi mwake, kwenda masharikini,
akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale; maji yakafika mpaka viweko vya miguu.
4 Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale, maji yakafika mpaka magoti.
Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha, maji yakafika mpaka viuno.
5 Kisha akapima dhiraa elfu, yakawa mto nisioweza kuuvuka; maana maji yamezidi,
maji ya kuogelea, mto usiovukika.
6 Akaniambia, Mwanadamu, je! Umeona haya? Kisha akanichukua akanirudisha mpaka
ukingo wa mto.
7 Basi nikiisha kurudi, tazama, kando ya ukingo wa mto ilikuwapo miti mingi sana,
upande huu na upande huu.
8 Ndipo akaniambia, Maji haya yanatoka kwenda pande za nchi ya mashariki, nayo
yanashuka mpaka Araba, na kuingia katika bahari maji yatokezwayo yataingia baharini, na maji yake yataponyeka.
9 Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo,
kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko maana
maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi po pote utakapofikilia mto huo.
10 Tena itakuwa, wavuvi watasimama karibu nao; toka Engedi mpaka En-eglaimu,
patakuwa ni mahali pa kutandazia nyavu; samaki wao watakuwa namna zao mbalimbali, kama
samaki wa bahari kubwa, wengi sana.
11 Bali mahali penye matope, na maziwa yake, hayataponywa; yataachwa yawe ya
chumvi.
12 Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti
wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe;
utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na
matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa.
13 Bwana MUNGU asema hivi; Huu ndio mpaka ambao mtaigawanya nchi iwe urithi
sawasawa na kabila kumi na mbili za Israeli; kwa Yusufu, mafungu mawili.
14 Nanyi mtaimiliki, mtu huyu sawasawa na huyu; ambayo naliuinua mkono wangu kuwapa
baba zenu; na nchi hii itawaangukia kuwa urithi.
15 Na huu ndio mpaka wa nchi; upande wa kaskazini, toka bahari kubwa, kwa njia ya
Hethloni, mpaka maingilio ya Sedada;
16 Hamathi, na Berotha, na Sibraimu, ulio katikati ya mpaka wa Dameski na mpaka wa
Hamathi; na Haser-hatikoni, ulio karibu na mpaka wa Haurani.
17 Nao mpaka toka baharini utakuwa Hasar-enoni, penye mpaka wa Dameski, na
kaskazini kuelekea upande wa kaskazini ndio mpaka wa Hamathi. Huu ndio upande wa
kaskazini.
18 Na upande wa mashariki, kati ya Haurani na Dameski, na Gileadi na nchi ya
Israeli, utakuwa mto Yordani; mtapima toka mpaka wa upande wa kaskazini hata bahari ya
mashariki. Huu ndio upande wa mashariki.
19 Na upande wa kusini, kuelekea kusini, utakuwa ni kutoka Tamari mpaka maji ya
Meriba-Kadeshi, mpaka kijito cha Misri, mpaka bahari kubwa. Huu ndio upande wa kusini,
kuelekea kusini.
20 Na upande wa magharibi, utakuwa ni bahari kubwa, kutoka mpaka wa kusini mpaka
mahali penye kuelekea maingilio ya Hamathi. Huu ndio upande wa magharibi.
21 Basi ndivyo mtakavyojigawanyia nafsi zenu nchi hii, sawasawa na kabila za
Israeli.
22 Tena itakuwa mtaigawanya kwa kura, kuwa urithi kwenu, na kwa wageni wakaao kwenu
hali ya ugeni, watakaozaa watoto kati yenu, nao watakuwa kwenu, kama wazaliwa miongoni
mwa wana Israeli; watakuwa na urithi pamoja nanyi kati ya kabila za Israeli.
23 Tena itakuwa, mgeni akaaye katika kabila iwayo yote, atapewa urithi katika
kabila asema Bwana MUNGU.