Ezekieli
Mlango 43
Kisha akanileta mpaka langoni, yaani, lango lile lielekealo upande wa mashariki;
2 na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na
sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling'aa kwa utukufu wake.
3 Na maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona nilipokuja kuuharibu mji;
nayo maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona karibu na mto wa Kebari;
nikaanguka kifudifudi.
4 Na huo utukufu wa Bwana ukaingia ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile
lielekealo upande wa mashariki.
5 Kisha Roho ikaniinua, ikanichukua mpaka ua wa ndani; na tazama, utukufu wa Bwana
uliijaza nyumba.
6 Nikasikia sauti ya mmoja asemaye nami, itokayo katika nyumba hiyo; na mtu
akasimama karibu nami.
7 Akaniambia, Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali pa nyayo
za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli milele; na nyumba ya Israeli
hawatalinajisi jina langu takatifu tena, wao, wala wafalme wao, kwa mambo yao ya
kikahaba, na kwa mizoga ya wafalme wao, katika mahali pao pa juu;
8 kwa kuweka kizingiti chao karibu na kizingiti changu; na mwimo wao karibu na
mwimo wangu; tena palikuwa na ukuta tu kati ya mimi na wao; nao wamelinajisi jina
langu takatifu kwa machukizo yao waliyoyatenda; basi, kwa sababu hiyo, nimewakomesha
katika hasira yangu.
9 Basi sasa wayaondoe mambo yao ya kikahaba, na mizoga ya wafalme wao, yawe mbali
nami, nami nitakaa kati yao milele.
10 Na wewe, mwanadamu, waonyeshe wana wa Israeli nyumba hii, ili wayatahayarikie
maovu yao; na waipime hesabu yake.
11 Na ikiwa wameyatahayarikia yote waliyoyatenda, waonyeshe umbo la nyumba, na
namna yake, na matokeo yake, na maingilio yake, na maumbo yake yote, na maagizo yake
yote, na kawaida zake zote, na sheria zake zote, ukayaandike machoni pao; ili
walishike umbo lake lote, na maagizo yake, na kuyatenda.
12 Hii ndiyo sheria ya nyumba; juu ya kilele cha mlima, mpaka wake wote pande zote
patakuwa patakatifu sana. Tazama, hii ndiyo sheria ya nyumba.
13 Na vipimo vya madhabahu kwa dhiraa ni hivi; (dhiraa ni dhiraa na shubiri); tako
lake ni dhiraa moja, na upana wake dhiraa moja; na pambizo yake karibu na ncha yake
pande zote, shubiri moja; na hili litakuwa tako la madhabahu.
14 Tena toka chini, juu ya nchi, hata daraja ya chini, dhiraa mbili, na upana wake
dhiraa moja; tena toka daraja ndogo hata daraja kubwa, dhiraa nne, na upana wake
dhiraa moja.
15 Na madhabahu ya juu itakuwa dhiraa nne; na toka madhabahu pawashwapo moto na
kwenda juu zitakuwa pembe nne.
16 Na pale pawashwapo moto, urefu wake dhiraa kumi na mbili, na upana wake kumi na
mbili, mraba pande zake nne.
17 Na daraja, urefu wake dhiraa kumi na nne, na upana wake dhiraa kumi na nne,
pande zake nne; na pambizo yake nusu dhiraa; na tako lake dhiraa moja, kote kote, na
madaraja yake yataelekea upande wa mashariki.
18 Kisha akaniambia, Mwanadamu, Bwana MUNGU asema hivi; Hizi ndizo sheria za
madhabahu katika siku ile watakapoifanya, ili watoe sadaka za kuteketezwa juu yake, na
kunyunyiza damu juu yake.
19 Utawapa makuhani Walawi, walio wa uzao wa Sadoki, walio karibu nami, ili
kunihudumu, asema Bwana MUNGU, ng'ombe mume mchanga awe sadaka ya dhambi.
20 Nawe utatwaa baadhi ya damu yake, na kuitia juu ya pembe zake nne, na juu ya
ncha nne za daraja, na juu ya pambizo yake pande zote; ndivyo utakavyoitakasa, na
kuifanyia upatanisho.
21 Tena utamtwaa ng'ombe wa sadaka ya dhambi, naye utamteketeza mahali palipoamriwa
pa nyumba ile, nje ya mahali patakatifu.
22 Na siku ya pili utamtoa beberu mkamilifu awe sadaka ya dhambi; nao wataisafisha
madhabahu, kama walivyoisafisha kwa ng'ombe huyo.
23 Utakapokwisha kuitakasa, utatoa ng'ombe mume mchanga mkamilifu, na kondoo mume
wa kundini mkamilifu.
24 Nawe utawaleta karibu mbele za Bwana, na makuhani watamwaga chumvi juu yao, nao
watawatoa wawe sadaka za kuteketezwa kwa Bwana.
25 Kwa muda wa siku saba utaweka tayari mbuzi kila siku awe sadaka ya dhambi; pia
wataweka tayari ng'ombe mume mchanga, na kondoo mume wa kundini, wakamilifu.
26 Kwa muda wa siku saba wataifanyia madhabahu upatanisho, na kuitakasa; ndivyo
watakavyoiweka wakfu.
27 Nao watakapozitimiza siku hizo, itakuwa, siku ya nane na baadaye, makuhani
watatoa sadaka zenu za kuteketezwa juu ya madhabahu, na sadaka zenu za amani nami
nitawakubali ninyi, asema Bwana MUNGU.