Ezekieli
Mlango 40
Katika mwaka wa ishirini na tano wa kuhamishwa kwetu, mwanzo wa mwaka, siku ya
kumi ya mwezi, katika mwaka wa kumi na nne baada ya kupigwa mji, siku iyo hiyo, mkono
wa Bwana ulikuwa juu yangu, akanileta huko.
2 Katika maono ya Mungu alinileta mpaka nchi ya Israeli, akaniweka juu ya mlima
mrefu sana, ambao juu yake palikuwapo kana kwamba ni umbo la mji upande wa kusini.
3 Akanileta huko, na tazama, alikuwapo mtu, ambaye kuonekana kwake kulikuwa kama
kuonekana kwa shaba, naye alikuwa na uzi wa kitani mkononi mwake, na mwanzi wa
kupimia; akasimama karibu na lango.
4 Mtu yule akaniambia, Mwanadamu, tazama kwa macho yako, sikia kwa masikio yako,
ukaweke moyoni mwako, yote nitakayokuonyesha; maana umeletwa hapa kusudi nikuonyeshe
haya; tangaza habari ya yote utakayoyaona kwa nyumba ya Israeli.
5 Na, tazama, kulikuwa na ukuta nje ya nyumba pande zote, na katika mkono wa mtu
yule mwanzi wa kupimia, urefu wake dhiraa sita, kila dhiraa, dhiraa na shubiri; basi
akaupima upana wa jengo lile, mwanzi mmoja, na urefu wake, mwanzi mmoja.
6 Kisha akaenda mpaka lango lielekealo upande wa mashariki, akapanda madaraja yake;
akakipima kizingiti cha lango; upana wake mwanzi mmoja; na kizingiti cha pili, upana
wake mwanzi mmoja.
7 Na kila chumba, upana wake mwanzi mmoja, na urefu wake mwanzi mmoja; na nafasi
iliyokuwa kati ya vyumba ni dhiraa tano; na kizingiti cha lango lililokuwa karibu na
ukumbi wa lango lililoielekea nyumba, mwanzi mmoja.
8 Akaupima na ukumbi wa lango lililoielekea nyumba, mwanzi mmoja.
9 Kisha akaupima ukumbi wa lango, dhiraa nane; na miimo yake, dhiraa mbili; na
ukumbi wa lango uliielekea nyumba.
10 Na vyumba vya walinzi, vya lango upande wa mashariki, vilikuwa vitatu upande
huu, na vitatu upande huu; vyote vitatu vya kipimo kimoja; nayo miimo ilikuwa na
kipimo kimoja, upande huu na upande huu.
11 Akaupima upana wa mahali pa kuliingilia lango, dhiraa kumi; na urefu wa lango,
dhiraa kumi na tatu.
12 Na mpaka, mbele ya vile vyumba, dhiraa moja upande huu, na mpaka, dhiraa moja
upande huu; na vile vyumba, dhiraa sita upande huu, na dhiraa sita upande huu.
13 Akalipima lango, toka paa la chumba kimoja hata paa la chumba cha pili, upana wa
dhiraa ishirini na tano; mlango mmoja ukielekea mlango wa pili.
14 Akafanya miimo pia, dhiraa sitini; na uwanda uliufikilia mwimo, lango lile
likizungukwa pande zote.
15 Na toka mahali palipo mbele ya lango, penye maingilio yake, hata mahali palipo
mbele ya ukumbi wa ndani ya lango, dhiraa hamsini.
16 Na kwa vile vyumba palikuwa na madirisha yaliyofungwa, na kwa miimo yake ndani
ya lango pande zote, na kwa matao yake vivyo hivyo; na madirisha yalikuwako, pande
zote upande wa ndani, tena palikuwa na mitende juu ya kila mwimo.
17 Ndipo akanileta mpaka ua wa nje, na tazama, palikuwa na vyumba, na sakafu
iliyofanyizwa kwa ule ua pande zote; vyumba thelathini vilikuwako juu ya sakafu ile.
18 Na ile sakafu ilikuwa kando ya malango, urefu wake sawasawa na urefu wa malango,
yaani, sakafu ya chini.
19 Kisha akaupima upana, toka mahali palipokuwa mbele ya lango la chini hata mahali
palipokuwa mbele ya ua wa ndani, nje yake, dhiraa mia upande wa mashariki, na upande
wa kaskazini.
20 Nalo lango la ua wa nje, lililoelekea kaskazini, akalipima urefu wake, na upana
wake.
21 Na vyumba vyake vya walinzi vilikuwa vitatu upande huu, na vitatu upande huu; na
miimo yake, na matao yake, kipimo chake ni sawasawa na kipimo cha lango la kwanza;
urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano.
22 Na madirisha yake, na matao yake, na mitende yake, kipimo chake ni sawasawa na
kipimo cha lango lililoelekea upande wa mashariki; nao hupanda kwa madaraja saba; na
matao yake yalikuwa mbele yake.
23 Na ule ua wa ndani ulikuwa na lango lililoelekea lile lango la pili, upande wa
kaskazini, na upande wa mashariki; akapima toka lango hata lango, dhiraa mia.
24 Akanileta mpaka upande wa kusini, na tazama, lango lililoelekea kusini; akaipima
miimo yake, na matao yake, sawasawa na vipimo hivyo.
25 Tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote kama
madirisha hayo; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano.
26 Tena palikuwa na madaraja saba ya kulipandia, na matao yake yalikuwa mbele yake;
nalo lilikuwa na mitende, mmoja upande huu, na mmoja upande huu, juu ya miimo yake.
27 Tena ua wa ndani ulikuwa na lango, lililoelekea kusini; akapima toka lango hata
lango, kwa kuelekea upande wa kusini, dhiraa mia.
28 Kisha akanileta mpaka ua wa ndani karibu na lango lililoelekea kusini; akalipima
lango la kusini kwa vipimo vivyo hivyo;
29 navyo vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake, sawasawa na vipimo
hivyo; tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote; urefu
wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano.
30 Tena palikuwa na matao pande zote, urefu wake dhiraa ishirini na tano na upana
wake dhiraa tano.
31 Na matao yake yaliuelekea ua wa nje, na mitende ilikuwa juu ya miimo yake;
palikuwa na madaraja manane ya kuupandia.
32 Akanileta mpaka ua wa ndani ulioelekea upande wa mashariki, akalipima lango kwa
vipimo vivyo hivyo;
33 navyo vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake, kwa vipimo hivyo;
tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote; urefu wake
dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano.
34 Na matao yake yaliuelekea ua wa nje; na mitende ilikuwa juu ya miimo yake,
upande huu na upande huu; tena palikuwa na madaraja manane ya kuupandia.
35 Akanileta mpaka lango lililoelekea upande wa kaskazini; akalipima kwa vipimo
vivyo hivyo;
36 vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake; tena palikuwa na
madirisha ndani yake pande zote; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa
ishirini na tano.
37 Na miimo yake iliuelekea ua wa nje; na mitende ilikuwa juu ya miimo yake, upande
huu na upande huu; tena palikuwa na madaraja manane ya kuupandia.
38 Na chumba, pamoja na lango lake, kilikuwa karibu na miimo ya malango; ndiko
walikoiosha sadaka ya kuteketezwa.
39 Na katika ukumbi wa lango palikuwa na meza mbili upande huu, na meza mbili
upande huu, ili kuichinja sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya dhambi, na sadaka ya
hatia.
40 Na upande mmoja, nje, penye madaraja ya kuliingia lango lililoelekea kaskazini,
palikuwa na meza mbili; na upande wa pili, ulio wa ukumbi wa lango hilo, palikuwa na
meza mbili.
41 Palikuwa na meza nne upande huu, na meza nne upande huu, karibu na lango; meza
nane ambazo juu yake walizichinja sadaka.
42 Tena palikuwa na meza nne kwa sadaka za kuteketezwa, za mawe yaliyochongwa;
urefu wake dhiraa moja na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kimo chake
dhiraa moja; juu yake waliviweka vyombo vya kuchinjia sadaka za kuteketezwa na sadaka.
43 Tena hizo kulabu, ambazo urefu wake ni shubiri, zilifungwa ndani pande zote; na
juu ya meza hizo ilikuwako nyama ya matoleo.
44 Tena nje ya lango la ndani palikuwa na vyumba kwa waimbaji, katika ua wa ndani,
uliokuwa kando ya lango lililoelekea kaskazini, navyo vilikabili upande wa kusini; na
kimoja kando ya lango lililoelekea upande wa mashariki, kilikabili upande wa
kaskazini.
45 Akaniambia, Chumba hiki kinachokabili upande wa kusini ni kwa makuhani, yaani,
hao walinzi wa malindo ya nyumba.
46 Nacho chumba kinachokabili upande wa kaskazini ni kwa makuhani, walinzi wa
malindo ya madhabahu; hao ni wana wa Sadoki, ambao miongoni mwa wana wa Lawi
wamkaribia Bwana, ili kumtumikia.
47 Akaupima huo ua, na urefu wake ulikuwa dhiraa mia, na upana wake dhiraa mia,
mraba; nayo dhabahu ilikuwa mbele ya nyumba.
48 Ndipo akanileta mpaka ukumbi wa nyumba, akapima kila mwimo wa ukumbi, dhiraa
tano upande huu, na dhiraa tano upande huu; na upana wa lango ulikuwa dhiraa tatu
upande huu, na dhiraa tatu upande huu.
49 Urefu wa ukumbi ulikuwa dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa kumi na moja;
karibu na madaraja ambayo waliupandia; tena palikuwa na nguzo karibu na miimo, moja
upande huu, na moja upande huu.