Ezekieli
Mlango 30
Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
2 Mwanadamu, tabiri, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Pigeni makelele ya uchungu, Ole
wa siku ile!
3 Kwa maana siku ile i karibu, siku ile ya Bwana i karibu, siku ya mawingu; itakuwa
wakati wa mataifa.
4 Na upanga utakuja juu ya Misri, na dhiki itakuwa katika Kushi, watakapoanguka
watu waliouawa katika Misri, nao watauondoa wingi wa watu wake, na misingi yake
itabomolewa.
5 Kushi, na Putu, na Ludi, na watu wote waliochanganyika, na Kubu, na wana wa nchi
ya agano, wataanguka kwa upanga pamoja nao.
6 Bwana asema hivi; Nao pia wanaoitegemeza Misri wataanguka, na kiburi cha uwezo
wake kitashuka; toka Migdoli hata Sewene, wataanguka ndani yake kwa upanga, asema
Bwana MUNGU.
7 Nao watakuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake itakuwamo kati ya
miji iliyoharibika.
8 Nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoweka moto katika Misri, na hao wote
wamsaidiao watakapoangamia.
9 Katika siku hiyo watatoka wajumbe mbele zangu katika merikebu, ili kuwatia hofu
Wakushi, wanaojiona kuwa salama, na dhiki itakuwa juu yao, vile vile kama katika siku
ya Misri; kwa maana, tazama, inakuja.
10 Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaukomesha wingi wa watu wa Misri, kwa mkono wa
Nebukadreza, mfalme wa Babeli.
11 Yeye, na watu wake pamoja naye, watu wa mataifa watishao, wataletwa waingie
katika nchi waiharibu, nao watafuta panga zao wapigane na Misri, na kuijaza nchi wale
waliouawa.
12 Nami nitaikausha mito, na kuiuza nchi, na kuitia katika mikono ya watu wabaya;
nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa, na watu wote walio ndani yake, kwa mkono wa wageni;
mimi, Bwana, nimenena neno hili.
13 Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaviharibu vinyago, nami nitavikomesha vitu vya
ubatili katika Nofu, wala hapatakuwa na mkuu tena atokaye katika nchi ya Misri, nami
nitatia hofu katika nchi ya Misri.
14 Nami nitaifanya Pathrosi kuwa ukiwa, nami nitatia moto katika Soani, nami
nitatekeleza hukumu katika No.
15 Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu ya Sini, ngome ya Misri, nami nitakatilia
mbali wingi wa watu wa No.
16 Nami nitatia moto katika Misri; Sini itakuwa katika dhiki kuu, na No itavunjika
kabisa; na Nofu itakuwa na adui wakati wa mchana.
17 Vijana wa Oni, na wa Pi-besethi, wataanguka kwa upanga; na miji hiyo itakwenda
utumwani.
18 Huko Tapanesi nako mchana utakuwa giza, nitakapovunja huko kongwa za Misri, na
kiburi cha uwezo wake kitakoma ndani yake, na katika habari zake, wingu litaifunika,
na binti zake watakwenda utumwani.
19 Hivyo ndivyo nitakavyotekeleza hukumu katika Misri; nao watajua ya kuwa mimi
ndimi Bwana.
20 Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, mwezi wa kwanza, siku ya saba ya mwezi,
neno la Bwana likanijia, kusema,
21 Mwanadamu, nimeuvunja mkono wa Farao, mfalme wa Misri, na tazama, haukufungwa
ili kuutia dawa, haukuzongwa kwa kitambaa, upate kuwa na nguvu za kushika upanga.
22 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya Farao, mfalme wa Misri, nami
nitamvunja mikono yake, mkono ulio wenye nguvu, na huo uliovunjika, nami nitauangusha
upanga ulio katika mkono wake.
23 Nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, na kuwatapanya kati ya nchi
mbalimbali.
24 Nami nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli, na kuutia upanga wangu katika
mkono wake, bali mikono ya Farao nitaivunja, naye ataugua mbele yake, kwa mauguzi ya
mtu aliyetiwa jeraha ya kumfisha.
25 Nami nitaitegemeza mikono ya mfalme wa Babeli, na mikono ya Farao itaanguka; nao
watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoutia upanga wangu katika mkono wa mfalme wa
Babeli, naye ataunyosha juu ya nchi ya Misri.
26 Nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, na kuwatapanya kati ya nchi
mbalimbali; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.