Isaya
Mlango 62
Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo.
2 Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha Bwana.
3 Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa Bwana, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako.
4 Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula; kwa kuwa Bwana anakufurahia, na nchi yako itaolewa.
5 Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe; na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.
6 Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha Bwana, msiwe na kimya;
7 wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani.
8 Bwana ameapa kwa mkono wake wa kuume, na kwa mkono wa nguvu zake, Hakika sitawapa adui zako nafaka yako tena kuwa chakula chao; wala wageni hawatakunywa divai yako, uliyoifanyia kazi.
9 Lakini walioivuna, ndio watakaoila, na kumhimidi Bwana; na walioichuma, ndio watakaoinywa, ndani ya nyua za patakatifu pangu.
10 Piteni, piteni, katika malango; Itengenezeni njia ya watu; Tutieni, tutieni barabara; toeni mawe yake; Twekeni bendera kwa ajili ya kabila za watu.
11 Tazama, Bwana ametangaza habari mpaka mwisho wa dunia, Mwambieni binti Sayuni, Tazama, wokovu wako unakuja; Tazama, thawabu yake i pamoja naye, Na malipo yake yako mbele zake.
12 Nao watawaita, Watu watakatifu, Waliokombolewa na Bwana; Nawe utaitwa, Aliyetafutwa, Mji usioachwa.