Isaya
Mlango 20
Katika mwaka ule jemadari Yule alipofika Ashdodi, alipotumwa na Sargoni mfalme wa Ashuru; naye alipigana na Ashdodi akautwaa.
2 wakati huo Bwana alinena kwa kinywa cha Isaya, mwana wa Amozi, akisema, Haya, uvue nguo ya magunia viunoni mwako, na viatu vyako miguuni mwako.
3 Naye akafanya hivyo akaenda uchi, miguu yake haina viatu. Bwana akasema, Kama vile mtumishi wangu Isaya anavyokwenda uchi, hana viatu, awe ishara na ajabu kwa muda wa miaka mitatu juu ya Misri na juu ya Kushi;
4 vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawachukua uchi, wafungwa wa Misri, na watu wa Kushi waliohamishwa, watoto kwa wazee, hawana viatu, matako yao wazi, Misri iaibishwe.
5 Nao watafadhaika, na kuona haya kwa ajili ya Kushi, matumaini yao, na Misri, utukufu wao.
6 Na mwenyeji wa nchi ya pwani atasema katika siku hiyo, Angalia, haya ndiyo yaliyowapata watu wale tuliowatumaini, ambao tuliwakimbilia watuokoe na mfalme wa Ashuru; na sisi je! Twawezaje kupona?