• Isaya Mlango 15
0:00
0:00

Mlango 15

Ufunuo juu ya Moabu. Maana katika usiku mmoja Ari wa Moabu umeharibiwa kabisa na kuangamizwa; maana katika usiku mmoja Kiri wa Moabu umeharibiwa kabisa na kuangamizwa.
2 Wanapanda juu hata Bayithi na Diboni, mpaka mahali palipo juu ili walie; juu ya Nebo na juu ya Medeba Wamoabi wanalia; Wana upaa juu ya vichwa vyao vyote; kila ndevu zimenyolewa.
3 Wanajivika nguo za magunia katika njia kuu zao; juu ya dari zao, na katika mitaa yao, kila mtu analia, anamwaga machozi.
4 Heshboni analia na Eleale; mpaka Yahasa sauti ya kulia kwao inasikiwa; hata watu wa Moabu waliovaa silaha wanapiga kelele sana kwa sababu hiyo; nafsi yake inatetemeka ndani yake.
5 Moyo wangu unamlilia Moabu; wakuu wake wanakimbilia Soari kama ndama wa miaka mitatu; kwa maana wanapanda mbavu za Luhithi wakilia; maana katika njia iendayo hata Horonaimu wanapaliza sauti ya kukata tamaa.
6 Kwa maana maji ya Nimrimu yamekuwa mahali palipoharibika, kwa kuwa majani yamekauka, miche imenyauka, majani mabichi yamekoma.
7 Kwa hiyo vitu walivyojipatia tele, na akiba yao, wanavichukua hata kijito cha mierebi.
8 Maana kilio hicho kimezunguka mipaka ya Moabu, malalamiko yao yamefika hata Eglaimu, na malalamiko yao hata Beer-Elimu.
9 Maana maji ya Dimoni yamejaa damu; maana ninaweka tayari msiba mpya juu ya Dimoni, simba juu ya watu wa Moabu waliokimbia, na juu ya mabaki yao.