Isaya
Mlango 1
Haya ni maono ya Isaya, mwana wa Amozi, aliyoyaona katika habari za Yuda na Yerusalemu, siku za Uzia na Yothamu na Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.
2 Sikieni, enyi mbingu, tega sikio, Ee nchi, kwa maana Bwana amenena; Nimewalisha watoto na kuwalea, nao wameniasi.
3 Ng'ombe amjua bwana wake, Na punda ajua kibanda cha bwana wake; Bali Israeli hajui, watu wangu hawafikiri.
4 Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha Bwana, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma.
5 Mbona mnataka kupigwa hata sasa, hata mkazidi kuasi? Kichwa chote ni kigonjwa, moyo wote umezimia.
6 Tangu wayo wa mguu hata kichwani hamna uzima ndani yake; bali jeraha na machubuko na vidonda vitokavyo usaha; havikufungwa, havikuzongwa-zongwa, wala havikulainishwa kwa mafuta.
7 Nchi yenu ni ukiwa; miji yenu imeteketezwa kwa moto; nchi yenu, wageni wameila mbele ya macho yenu; nayo ni ukiwa, kana kwamba imeangamizwa na wageni.
8 Na binti Sayuni ameachwa kama kibanda katika shamba la mizabibu, kama kipenu katika shamba la matango, kama mji uliohusuriwa.
9 Kama Bwana wa majeshi asingalituachia mabaki machache sana, tungalikuwa kama Sodoma, tungalifanana na Gomora.
10 Lisikieni neno la Bwana, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora.
11 Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema Bwana. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo waume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahii damu ya ng'ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi waume.
12 Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliyetaka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu?
13 Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada.
14 Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua.
15 Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu.
16 Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;
17 jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.
18 Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.
19 Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;
20 bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.
21 Mji huu uliokuwa mwaminifu umekuwaje kahaba! Yeye aliyejaa hukumu ya haki; haki ilikaa ndani yake, bali sasa wauaji!
22 Fedha yako imekuwa takataka, divai yako imechanganywa na maji.
23 Wakuu wako ni waasi, na rafiki za wevi; kila mtu hupenda rushwa, hufuata malipo; hawampatii yatima haki yake, wala maneno ya mjane hayawawasilii.
24 Kwa hiyo, asema Bwana, Bwana wa majeshi, Mwenye enzi, wa Israeli, Nitapata faraja kwa hao wanipingao, nitatwaa kisasi kwa adui zangu;
25 nami nitakuelekezea wewe mkono wangu, na kukutakasa takataka zako kabisa, na kukuondolea bati lako lote;
26 nami nitarejeza upya waamuzi wako kama walivyokuwa hapo kwanza, na washauri wako kama hapo mwanzo; baada ya hayo utaitwa, Mji wa haki, mji mwaminifu.
27 Sayuni itakombolewa kwa hukumu, na waongofu wake kwa haki.
28 Lakini kuharibika kwao wakosao nao wenye dhambi kutatokea wakati mmoja, nao wamwachao Bwana watateketezwa.
29 Kwa maana watatahayarika kwa sababu ya mialoni mliyoitamani, nanyi mtaaibishwa kwa sababu ya bustani mlizozichagua.
30 Maana mtakuwa kama mwaloni ambao majani yake yakauka, na kama bustani isiyo na maji.
31 Na mtu hodari atakuwa kama makumbi, na kazi yake kama cheche ya moto; nao watawaka pamoja, wala hapana atakayewazima.