Mithali
Mlango 19
Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake, Kuliko mpotofu wa midomo aliye mpumbavu.
2 Tena si vizuri nafsi ya mtu ikose maarifa; Naye afanyaye haraka kwa miguu hutenda dhambi.
3 Upumbavu wa mtu hupotosha njia yake; Na moyo wake hununa juu ya Bwana.
4 Utajiri huongeza rafiki wengi; Bali maskini hutengwa na rafiki yake.
5 Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa; Wala asemaye uongo hataokoka.
6 Watu wengi watamsihi mkuu ili awafadhili; Na kila mtu ni rafiki yake atoaye tunu.
7 Ndugu zote wa maskini humchukia; Jinsi gani rafiki zake huzidi kujitenga naye! Huwafuata kwa maneno, lakini wametoweka.
8 Apataye hekima hujipenda nafsi yake; Ashikaye ufahamu atapata mema.
9 Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa; Naye asemaye uongo ataangamia.
10 Maisha ya anasa hayampasi mpumbavu; Sembuse mtumwa awatawale wakuu.
11 Busara ya mtu huiahirisha hasira yake; Nayo ni fahari yake kusamehe makosa.
12 Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba; Bali hisani yake kama umande juu ya majani.
13 Mwana mpumbavu ni msiba kwa babaye; Na ugomvi wa mke kama kutona-tona daima.
14 Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.
15 Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito; Na nafsi yake mvivu itaona njaa.
16 Yeye aihifadhiye amri huihifadhi nafsi yake; Bali yeye asiyeziangalia njia zake atakufa.
17 Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana; Naye atamlipa kwa tendo lake jema.
18 Mrudi mwanao, kwa maana liko tumaini; Wala usiikaze nafsi yako kwa kuangamia kwake.
19 Mtu wa hasira nyingi atachukua adhabu yake, Maana ujapomwokoa huna budi kufanya tena.
20 Sikiliza mashauri, ukapokee mafundisho, Upate kuwa na hekima siku zako za mwisho.
21 Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama.
22 Haja ya mwanadamu ni hisani yake; Ni afadhali maskini kuliko mwongo.
23 Kumcha Bwana huelekea uhai; Atakaa ameshiba; hatajiliwa na ubaya.
24 Mtu mvivu hutia mkono wake sahanini; Ila hataki hata kuupeleka kinywani pake.
25 Mpige mwenye mzaha, na mjinga atapata busara; Mwonye mwenye ufahamu, naye atatambua maarifa.
26 Apotezaye mali za babaye na kumfukuza mamaye, Ni mwana aaibishaye, na kuleta lawama.
27 Mwanangu, acha kusikia mafundisho, Ukitaka tu kuyaasi maneno ya maarifa.
28 Shahidi asiyefaa kitu hudhihaki hukumu, Na vinywa vya wasio haki humeza uovu.
29 Hukumu zimewekwa tayari kwa wenye mzaha; Na mapigo kwa mgongo wa wapumbavu.