0:00
0:00

Mlango 15

Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.
2 Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri; Bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu.
3 Macho ya Bwana yako kila mahali; Yakimchunguza mbaya na mwema.
4 Ulimi safi ni mti wa uzima; Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo.
5 Mpumbavu hudharau kurudiwa na babaye; Bali yeye aangaliaye maonyo hupata busara.
6 Katika nyumba ya mwenye haki mna akiba nyingi; Bali mapato ya mtu mbaya huwa taabu tu.
7 Midomo ya mwenye haki hueneza maarifa; Bali moyo wa mpumbavu haufanyi hivyo.
8 Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake.
9 Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali humpenda mtu afuatiaye wema.
10 Adhabu kali ina yeye aiachaye njia; Naye achukiaye kukemewa atakufa.
11 Kuzimu na Uharibifu vi wazi mbele za Bwana; Si zaidi basi, mioyo ya wanadamu?
12 Mwenye mzaha hapendi kukaripiwa; Wala yeye hawaendei wenye hekima.
13 Moyo wa furaha huchangamsha uso; Bali kwa huzuni ya moyo roho hupondeka.
14 Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa; Bali kinywa cha wapumbavu hula upumbavu.
15 Siku zote za mtu ateswaye ni mbaya; Bali ukunjufu wa moyo ni karamu ya daima.
16 Kuwa na mali chache pamoja na kumcha Bwana; Ni bora kuliko mali nyingi pamoja na taabu.
17 Chakula cha mboga penye mapendano; Ni bora kuliko ng'ombe aliyenona pamoja na kuchukiana.
18 Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano.
19 Njia ya mtu mvivu ni kama boma la miiba; Bali mapito yao wenye unyofu hufanyika njia kuu.
20 Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mpumbavu humdharau mamaye.
21 Upumbavu ni furaha kwake aliyepungukiwa na akili; Bali mwenye ufahamu huunyosha mwenendo wake.
22 Pasipo mashauri makusudi hubatilika; Bali kwa wingi wa washauri huthibithika.
23 Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake; Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini!
24 Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu; Ili atoke katika kuzimu chini.
25 Bwana ataing'oa nyumba ya mwenye kiburi; Bali atauthibitisha mpaka wa mjane.
26 Mashauri mabaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maneno yapendezayo ni safi.
27 Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe; Bali achukiaye zawadi ataishi.
28 Moyo wa mwenye haki hufikiri jinsi atakavyojibu; Bali kinywa cha wasio haki humwaga mabaya.
29 Bwana yu mbali na wasio haki; Bali huisikia sala ya mwenye haki.
30 Mng'ao wa macho huufurahisha moyo; Habari njema huinenepesha mifupa.
31 Sikio lisikilizalo lawama yenye uhai Litakaa kati yao wenye hekima.
32 Akataaye maonyo huidharau nafsi yake mwenyewe; Bali yeye asikilizaye lawama hujipatia ufahamu.
33 Kumcha Bwana ni maonyo ya hekima; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.