0:00
0:00

Mlango 12

Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa; Bali yeye achukiaye kulaumiwa ni kama mnyama.
2 Mtu mwema atapata upendeleo kwa Bwana; Bali mtu wa hila atahukumiwa naye.
3 Mtu hatathibitika kwa njia ya uovu; Shina la mwenye haki halitaondolewa kamwe.
4 Mwanamke mwema ni taji ya mumewe; Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake.
5 Mawazo ya mwenye haki ni adili; Bali mashauri ya mtu mwovu ni hadaa.
6 Maneno ya waovu huotea damu; Bali kinywa cha wanyofu kitawaokoa.
7 Waovu huangamia, hata hawako tena; Bali nyumba ya mwenye haki itasimama.
8 Mtu atasifiwa kwa kadiri ya akili zake; Bali mwenye moyo wa ukaidi atadharauliwa.
9 Afadhali mtu anayedharauliwa, ikiwa ana mtumwa, Kuliko ajisifuye, ikiwa anahitaji chakula.
10 Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake; Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili.
11 Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi hana ufahamu.
12 Asiye haki hutamani nyavu za wabaya; Bali shina lao wenye haki huleta matunda.
13 Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya; Bali mwenye haki atatoka katika taabu.
14 Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake; Na atarudishiwa matendo ya mikono yake.
15 Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.
16 Ghadhabu ya mpumbavu hujulika mara; Bali mtu mwerevu husitiri aibu.
17 Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo hutamka hila.
18 Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; Bali ulimi wa mwenye haki ni afya.
19 Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.
20 Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu; Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha.
21 Mwenye haki hatapatikana na msiba wo wote; Bali wasio haki watajazwa mabaya.
22 Midomo ya uongo ni chukizo kwa Bwana; Bali watendao uaminifu ndio furaha yake.
23 Mwanadamu mwenye busara husitiri maarifa; Bali moyo wa wapumbavu hutangaza upumbavu.
24 Mkono wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipishwa kodi.
25 Uzito katika moyo wa mtu huuinamisha; Bali neno jema huufurahisha.
26 Mwenye haki ni kiongozi cha mwenzake; Bali njia ya wasio haki huwakosesha.
27 Mtu mvivu hapiki mawindo yake; Bali mwenye bidii anazo mali za thamani.
28 Katika njia ya haki kuna uhai; Wala hakuna mauti katika mapito yake.