Ayubu
Mlango 7
Je! Mtu hana wakati wake wa vita juu ya nchi? Na siku zake, je! Si kama siku za mwajiriwa?
2 Kama mtumishi atamaniye sana kile kivuli, Kama mwajiriwa anayetazamia mshahara wake;
3 Ni vivyo nami nimepewa miezi ya ubatili iwe fungu langu, Nami nimeandikiwa masiku yenye kuchokesha.
4 Hapo nilalapo chini, nasema, Nitaondoka lini? Lakini usiku huwa mrefu; Nami nimejawa na kujitupa huku na huku hata kupambazuke.
5 Mwili wangu unavikwa mabuu na madongoa ya udongo; Ngozi yangu hufumba, kisha ikatumbuka tena.
6 Siku zangu hupita upesi kuliko chombo cha kufumia, Nazo zapita pasipokuwa na matumaini.
7 Kumbuka ya kwamba maisha yangu ni upepo; Jicho langu halitaona mema tena.
8 Jicho lake huyo anionaye halitaniangalia tena; Macho yako yatanielekea, lakini sitakuwapo.
9 Kama vile wingu likomavyo na kutoweka, Ni vivyo huyo ashukaye kuzimuni hatazuka tena kabisa.
10 Hatarudi tena nyumbani kwake, Wala mahali pake hapatamjua tena.
11 Kwa hiyo sitakizuia kinywa changu; Nitanena kwa mateso ya roho yangu; Nitalia kwa uchungu wa nafsi yangu.
12 Je! Mimi ni bahari, au je! Ni nyangumi? Hata ukawaweka walinzi juu yangu?
13 Hapo nisemapo, kitanda changu kitanituza moyo, Malazi yangu yatanipunguzia kuugua kwangu;
14 Ndipo unitishapo kwa ndoto, Na kunitia hofu kwa maono;
15 Hata nafsi yangu huchagua kunyongwa, Na kuchagua kifo kuliko maumivu yangu haya.
16 Ninadhoofika; sitaishi sikuzote; Usinisumbue, kwani siku zangu ni uvuvio.
17 Je! Mtu ni kitu gani, hata ukamtukuza, Na kumtia moyoni mwako,
18 Na kumwangalia kila asubuhi, Na kumjaribu kila dakika?
19 Je! Hata lini hukomi kuniangalia; Wala kunisumbua hata nimeze mate?
20 Kwamba nimefanya dhambi, nikufanyieje Ee mlinda wanadamu? Mbona umeniweka niwe shabaha yako, Hata nimekuwa mzigo kwa nafsi yangu?
21 Nawe, je! Mbona hunisamehe makosa yangu, Na kuniondolea maovu yangu? Kwa kuwa sasa nitalala mavumbini; Nawe utanitafuta kwa bidii, lakini sitakuwapo.