Ayubu
Mlango 27
Kisha Ayubu akaendelea na mithali yake, na kusema,
2 Kama aishivyo Mungu, aliyeniondolea haki yangu; Huyo Mwenyezi aliyeitesa nafsi yangu;
3 (Kwa kuwa uhai wangu ukali mzima ndani yangu, Na roho ya Mungu i katika pua yangu;)
4 Hakika midomo yangu haitanena yasiyo haki, Wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu.
5 Hasha! Nisiwahesabie ninyi kuwa na haki; Hata nitakapokufa sitajiondolea uelekevu wangu.
6 Haki yangu naishika sana, wala sitaiacha; Moyo wangu hautanisuta wakati nikiwapo hai.
7 Adui yangu na awe kama huyo mwovu, Na mwenye kuondoka kinyume changu na awe kama asiye haki.
8 Kwani tumaini la mpotovu ni nini, ingawa ajipatia faida, Hapo Mungu amwondoleapo roho yake?
9 Je! Mungu atakisikia kilio chake, Taabu zitakapomfikilia?
10 Je! Atajifurahisha katika Mwenyezi, Na kumlingana Mungu nyakati zote?
11 Nitawafundisha ninyi mambo ya mkono wa Mungu; Hayo yaliyo kwa Mwenyezi sitayaficha.
12 Tazama, ninyi nyote mmeyaona wenyewe; Mbona basi mmebatilika kabisa?
13 Hii ndiyo sehemu ya mtu mwovu kwa Mungu, Na urithi wa hao waoneao, waupokeao kwa Mwenyezi.
14 Watoto wake wakiongezeka ni kwa upanga; Na wazao wake hawatashiba chakula.
15 Hao watakaosalia kwake watazikwa katika kufa, Wala wajane wake waliofiwa na waume hawataomboleza.
16 Ajapokusanya fedha kama mavumbi, Na kujifanyia mavazi kama udongo kwa wingi;
17 Yumkini kuyatengeza, lakini wenye haki watayavaa, Nao wasio na hatia watazigawanya hizo fedha.
18 Yeye hujenga nyumba yake kama mdudu, Na kama kibanda afanyacho mlinzi.
19 Yeye hujilaza hali ni tajiri, lakini ndio mwisho; Hufunua macho yake, naye hayuko.
20 Vitisho vyampata kama maji mengi; Dhoruba humwiba usiku.
21 Upepo wa mashariki humchukua, naye huondoka; Na kumkumba atoke mahali pake.
22 Kwani Mungu atamtupia asimhurumie; Angependa kuukimbia mkono wake.
23 Watu watampigia makofi, Na kumzomea atoke mahali pake.