Ayubu
Mlango 10
Nafsi yangu inachoka na maisha yangu; Sitajizuia na kuugua kwangu; Nitanena kwa uchungu wa roho yangu.
2 Nitamwambia Mungu, Usinihukumie makosa; Nionyeshe sababu ya wewe kushindana nami.
3 Je! Ni vema kwako wewe kuonea, Na kuidharau kazi ya mikono yako, Na kuyaangazia mashauri ya waovu?
4 Je! Wewe una macho ya kimwili, Au je! Waona kama aonavyo binadamu?
5 Je! Siku zako ni kama siku za mtu, Au je! Miaka yako ni kama siku za mtu,
6 Hata ukauliza-uliza habari za uovu wangu, Na kuitafuta dhambi yangu,
7 Ujapojua ya kuwa mimi si mwovu; Wala hapana awezaye kuokoa na mkono wako?
8 Mikono yako imeniumba na kunifinyanga; Nawe utageuka na kuniangamiza?
9 Kumbuka, nakusihi ulivyonifinyanga kama vile udongo; Nawe, je! Utanirudisha uvumbini tena?
10 Je! Wewe hukunimimina kama maziwa, Na kunigandisha mfano wa jibini?
11 Umenivika ngozi na nyama, Na kuniunga pamoja kwa mifupa na mishipa.
12 Umenijazi uhai na upendeleo, Na maangalizi yako yameilinda roho yangu.
13 Lakini mambo haya uliyaficha moyoni mwako; Najua kuwa haya yamo nafsini mwako;
14 Nikifanya dhambi, ndipo waniangalia, Wala hutaniachilia na uovu wangu.
15 Mimi nikiwa mbaya, ole wangu! Nami nikiwa mwenye haki, walakini sitainua kichwa changu; Mimi nimejaa aibu Na kuyaangalia mateso yangu.
16 Kichwa changu kikijiinua, waniwinda kama simba; Tena wajionyesha kwangu kuwa wa ajabu.
17 Wewe warejeza upya hao mashahidi yako juu yangu, Na kasirani yako waiongeza juu yangu; Jeshi kwa jeshi juu yangu.
18 Kwa nini basi kunitoa tumboni? Ningekata roho, lisinione jicho lo lote.
19 Ningalikuwa kama mtu asiyekuwapo; Ningalichukuliwa kaburini kutoka tumboni.
20 Je! Siku zangu si chache? Acha basi, Usinisumbue, nipate ngaa kutuzwa moyo kidogo.
21 Kabla sijaenda huko ambako sitarudi kutoka huko tena, Ni hiyo nchi ya giza, giza tupu;
22 Ni nchi ya giza kuu, kama giza lenyewe lilivyo; Ni nchi ya giza tupu, isiyo na matengezo ya mambo yo yote, Nchi ambayo nuru yake ni kama giza.