0:00
0:00

Mlango 9

Ikawa Sulemani alipokwisha kuijenga nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme, na mambo yote yaliyoingia moyoni mwake Sulemani, naye akataka kuyafanya,
2 basi, Bwana akamtokea Sulemani mara ya pili kama alivyomtokea huko Gibeoni.
3 Bwana akamwambia, Nimeyasikia maombi yako na dua zako, ulizotoa mbele zangu. Nimeitakasa nyumba hii uliyoijenga ili niweke jina langu humo milele; tena macho yangu na moyo wangu utakuwapo hapo siku zote;
4 na wewe, ukienda mbele zangu kama alivyokwenda Daudi, baba yako, kwa ukamilifu wa moyo, na kwa adili, kufanya hayo yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu,
5 ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli.
6 Bali mkighairi, mkaacha kunifuata, ninyi na watoto wenu, msizishike sheria zangu na amri zangu, nilizoziweka mbele yenu, tena mkienda na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu,
7 basi nitawakatilia Israeli mbali na nchi hii niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaitupilia mbali na macho yangu, na Israeli watakuwa mithali na neno la tusi katika mataifa yote.
8 Na ijapokuwa nyumba hii imetukuka namna hii, lakini kila apitaye atasituka na kuizomea; nao watasema, Kwa nini Bwana ameitenda nchi hii na nyumba hii mambo haya?
9 Na watu watajibu, Kwa sababu walimwacha Bwana, Mungu wao, aliyewatoa baba zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine na kuiabudu na kuitumikia, basi ndiyo sababu Bwana ameleta mabaya haya yote juu yao.
10 Ikawa miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani alizijenga zile nyumba mbili, nyumba ya Bwana na nyumba yake mfalme,
11 (basi Hiramu, mfalme wa Tiro, alikuwa amemletea Sulemani mierezi na miberoshi, na dhahabu, sawasawa na haja zake zote), ndipo mfalme Sulemani akampa Hiramu miji ishirini ya nchi ya Galilaya.
12 Naye Hiramu akatoka Tiro kuitazama hiyo miji Sulemani aliyompa; wala haikumpendeza.
13 Akasema, Miji gani hii uliyonipa, ndugu yangu? Akaiita nchi ya Kabuli, hata leo.
14 Hiramu akamletea mfalme talanta sitini za dhahabu.
15 Na hii ndiyo sababu ya shokoa aliyoitoza mfalme Sulemani; ili kuijenga nyumba ya Bwana, na nyumba yake mwenyewe, na Milo, na ukuta wa Yerusalemu, na Hazori, na Megido, na Gezeri.
16 Farao, mfalme wa Misri, alikuwa amepanda akautwaa Gezeri, na kuuteketeza kwa moto, akawaua Wakanaani waliokaa mjini, akampa zawadi binti yake, mkewe Sulemani.
17 Naye Sulemani akaujenga Gezeri, na Beth-horoni wa chini,
18 na Baalathi, na Tamari ulio nyikani, katika nchi;
19 na miji yote ya hazina iliyokuwa yake Sulemani; na miji ya magari yake, na miji ya watu wake wapandao farasi, na kila alichopenda kujenga Sulemani huko Yerusalemu, na katika Lebanoni, na katika nchi yote ya mamlaka yake.
20 Kwa habari ya watu wote waliosalia, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi, wasiokuwa wa wana wa Israeli;
21 watoto wao waliosalia baada yao katika nchi, ambao wana wa Israeli hawakuweza kuwaharibu kabisa, katika hao Sulemani akawatumikisha shokoa hata leo.
22 Lakini wa wana wa Israeli Sulemani hakumtumikisha mtu shokoa; ila ndio watu wa vita, na wangoje wake, na wakuu wake, na akida zake, na wakuu, wa magari yake, na wa wapanda farasi wake.
23 Hao maakida wakuu, waliokuwa juu ya kazi yake Sulemani, walikuwa mia tano na hamsini, waliowaamuru watu watendao kazi.
24 Lakini binti Farao akapanda toka mji wa Daudi, mpaka hiyo nyumba yake Sulemani, aliyomjengea; kisha, aliijenga Milo.
25 Na mara tatu kila mwaka Sulemani alikuwa akitoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani juu ya madhabahu aliyomjengea Bwana akafukiza uvumba pamoja nazo juu ya madhabahu iliyokuwako mbele za Bwana. Hivyo akaimaliza nyumba.
26 Tena, mfalme Sulemani akaunda merikebu huko Ezion-geberi, ulioko karibu na Elothi, pwani ya Bahari ya Shamu, katika nchi ya Edomu.
27 Naye Hiramu akatuma merikebuni watumishi wake, wanamaji wenye kuijua bahari, pamoja na watumishi wake Sulemani.
28 Wakafika Ofiri, wakachukua toka huko dhahabu, talanta mia nne na ishirini, wakamletea mfalme Sulemani.