0:00
0:00

Mlango 19

Basi, Ahabu akamwambia Yezebeli habari ya mambo yote aliyoyafanya Eliya, na jinsi alivyowaua manabii wote kwa upanga.
2 Ndipo Yezebeli akampelekea Eliya mjumbe, kusema, Miungu wanifanyie hivyo na kuzidi, nisipokufanya roho yako kesho, panapo wakati huu, kama roho ya mmojawapo wa hao.
3 Naye alipoona hayo, aliondoka, akaenda aihifadhi roho yake, akafika Beer-sheba, mji wa Yuda, akamwacha mtumishi wake huko.
4 Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu.
5 Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule.
6 Akatazama, kumbe! Pana mkate umeokwa juu ya makaa, na gudulia la maji, kichwani pake. Akala, akanywa, akajinyosha tena.
7 Malaika wa Bwana akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, Inuka, ule; maana safari hii ni kubwa mno kwako.
8 Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu.
9 Akafika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la Bwana likamjia, naye akamwambia, Unafanya nini hapa, Eliya?
10 Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu, waiondoe.
11 Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi;
12 na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu.
13 Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama, sauti ikamjia, kusema, Unafanya nini hapa, Eliya?
14 Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana, Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu waiondoe.
15 Bwana akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu.
16 Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako.
17 Na itakuwa atakayeokoka na upanga wa Hazaeli, Yehu atamwua; na atakayeokoka na upanga wa Yehu, Elisha atamwua.
18 Pamoja na hayo nitajisazia katika Israeli watu elfu saba, kila goti lisilomwinamia Baali, na kila kinywa kisichombusu.
19 Basi, akaondoka huko, akamkuta Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akilima, mwenye jozi za ng'ombe kumi na mbili mbele yake, na yeye mwenyewe alikuwa pamoja na lile la kumi na mbili. Eliya akapita karibu naye, akatupa vazi lake juu yake.
20 Naye akawaacha ng'ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata. Akamwambia, Enenda, urudi; ni nini niliyokutendea?
21 Akarudi akiacha kumfuata, akatwaa lile jozi la ng'ombe, akawachinja, akatokosa nyama zao kwa ile miti ya ng'ombe, akawapa watu, wakala. Kisha akainuka, akamfuata Eliya, akamhudumia.