1 Wafalme
Mlango 4
Basi mfalme Sulemani akawa mfalme juu ya Israeli wote.
2 Na hawa ndio wakuu aliokuwa nao; Azaria mwana wa Sadoki, kuhani,
3 Elihorefu na Ahiya, wana wa Shausha, waandishi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi mwenye kuandika tarehe;
4 na Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya jeshi; na Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani;
5 na Azaria mwana wa Nathani alikuwa juu ya maakida; na Zabudi mwana wa Nathani alikuwa kuhani, rafiki wake mfalme.
6 Na Ahishari alikuwa juu ya nyumba; na Adoramu mwana wa Abda alikuwa juu ya shokoa.
7 Sulemani alikuwa na maakida kumi na wawili juu ya Israeli wote, walioleta chakula cha mfalme na nyumba yake; kila mtu alikuwa na mwezi mmoja katika mwaka kuleta chakula.
8 Na haya ndiyo majina yao. Mwana wa Huri, mlimani mwa Efraimu.
9 Mwana wa Dekari, kutoka Makasi, na Shaalbimu na Bethshemeshi na Elon-beth-hanani.
10 Mwana wa Hesedi, katika Arubothi; na Soko ilikuwa kwake na nchi yote ya Heferi.
11 Mwana wa Abinadabu katika Nafath-dori yote; ndiye aliyekuwa naye Tafathi binti Sulemani kuwa mke wake.
12 Baana mwana wa Ahiludi, katika Taanaki na Megido, na Beth-sheani yote, iliyo kando ya Sarethani, chini ya Yezreeli, tangu Beth-sheani mpaka Abel-mehola, hata kupita Yokmeamu.
13 Mwana wa Geberi katika Ramoth-gileadi; na kwake ilikuwa miji ya Yairi mwana wa Manase iliyomo Gileadi; na kwake ilikuwa wilaya ya Argobu, iliyomo Bashani, miji mikubwa sitini yenye kuta na makomeo ya shaba.
14 Ahinadabu mwana wa Ido, katika Mahanaimu.
15 Ahimaasi, katika Naftali; naye ndiye aliyemwoa Basemathi binti Sulemani.
16 Baana mwana wa Hushai, katika Asheri na Bealothi.
17 Yehoshafati mwana wa Parua, katika Isakari.
18 Shimei mwana wa Ela, katika Benyamini.
19 Geberi mwana wa Uri, katika nchi ya Gileadi, nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, na Ogu mfalme wa Bashani; naye alikuwa akida wa pekee katika nchi hiyo.
20 Yuda na Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani kwa wingi, wakila, na kunywa, na kufurahi.
21 Sulemani akatawala juu ya falme zote, toka Mto mpaka nchi ya Wafilisti, na hata mpaka wa Misri; walimletea tunu, na kumtumikia Sulemani siku zote za maisha yake.
22 Na vyakula vya Sulemani vya siku moja vilikuwa kori therathini za unga wa mzuri, na kori sitini za ngano.
23 na ng'ombe kumi walionona, na ng'ombe ishirini za malisho, na kondoo mia, pamoja na ayala, na paa, na kulungu, na kuku walionona.
24 Kwani alikuwa akitawala nchi yote upande huu wa Mto, toka Tifsa mpaka Gaza, juu ya wafalme wote wa upande huu wa Mto; naye alikuwa na amani pande zake zote.
25 Yuda na Israeli wakakaa salama, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, tokea Dani mpaka Beer-sheba, siku zote za Sulemani.
26 Tena Sulemani alikuwa na mabanda ya farasi arobaini elfu kwa magari yake, na wapandao farasi kumi na mbili elfu.
27 Na maakida wale wakaleta chakula kwa mfalme Sulemani na kwa wote walioijia meza ya mfalme Sulemani, kila mtu katika mwezi wake, kisipunguke kitu.
28 Shayiri pia na majani kwa farasi, na kwa wanyama wenye mbio, wakaleta mahali walipokuwapo, kila mtu kwa kadiri ya kazi yake.
29 Mungu akampa Sulemani hekima, na akili nyingi sana, na moyo mkuu, kama mchanga ulioko pwani.
30 Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya wana wote wa mashariki, na hekima zote za Misri.
31 Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote; kuliko Ethani Mwezrahi, na Hemani, na Kalkoli, na Darda, wana wa Maholi; zikaenea sifa zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka.
32 Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano.
33 Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki.
34 Wakaja wa mataifa yote ili waisikie hekima ya Sulemani, toka wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamepata habari za hekima yake.