0:00
0:00

Mlango 14

Siku zile akaugua Abiya, mwana wa Yeroboamu.
2 Yeroboamu akamwambia mkewe, Ondoka, tafadhali, ujibadilishe, wasikujue kuwa mkewe Yeroboamu; ukaende Shilo; tazama, yuko huko Ahiya nabii, aliyeninena mimi ya kwamba nitakuwa mfalme juu ya watu hawa.
3 Twaa mkononi mikate kumi, na kaki, na mtungi wa asali, ukamwendee; naye atakuambia kijana atakuwaje.
4 Akafanya hivi mkewe Yeroboamu, akaondoka, akaenda Shilo, akaja nyumbani kwa Ahiya. Basi Ahiya hakuweza kuona; kwa kuwa macho yake yamepofuka kwa sababu ya uzee wake.
5 Bwana akamwambia Ahiya, Angalia, mkewe Yeroboamu anakuja akuulize mambo ya mwanawe; kwa maana hawezi; hivi na hivi umwambie; kwani itakuwa akiingia atajifanya kuwa mwanamke mwingine.
6 Ikawa, Ahiya alipoisikia sauti ya miguu yake, akiingia mlangoni, alisema, Karibu, mkewe Yeroboamu; mbona wajifanya kuwa mwingine maana nimetumwa kwako wewe, mwenye maneno mazito.
7 Nenda, umwambie Yeroboamu, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa nilikutukuza miongoni mwa watu, nikakufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli,
8 nikaurarulia mbali ufalme utoke nyumba yake Daudi, na kukupa wewe; walakini wewe hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, aliyezishika amri zangu, na kunifuata kwa moyo wake wote, asifanye lo lote ila yaliyo mema machoni pangu;
9 lakini umekosa kuliko wote waliokutangulia, umekwenda kujifanyia miungu mingine, na sanamu zilizoyeyuka, unikasirishe, na kunitupa nyuma yako;
10 tazama, kwa hiyo mimi nitaleta mabaya juu ya nyumba yake Yeroboamu, nami nitamkatia Yeroboamu kila mwanamume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli, nami kuondoa nitawaondoa waliobaki wa nyumba yake Yeroboamu, kama mtu aondoavyo mavi, hata itakapokwisha pia.
11 Yeye afaye wa Yeroboamu mjini mbwa watamla; afaye mashambani ndege wa angani watamla; kwa kuwa Bwana amelinena hilo.
12 Basi ondoka, urudi nyumbani kwako; na miguu yako itakapoingia mjini huyo kijana atakufa.
13 Na Israeli wote watamlilia, na kumzika, kwa maana ndiye peke yake wa Yeroboamu atakayeingia kaburini; kwa sababu limeonekana ndani yake jambo lililo jema kwa Bwana, Mungu wa Israeli, nyumbani mwa Yeroboamu.
14 Tena Bwana atajiinulia mfalme wa Israeli atakayeiharibu nyumba ya Yeroboamu siku ile; na nini tena hata sasa?
15 Kwa kuwa Bwana atawapiga Israeli kama manyasi yatikiswavyo majini; naye atawang'oa Israeli katika nchi hii njema, aliyowapa baba zao, naye atawatawanya ng'ambo ya Mto; kwa sababu wamejifanyia maashera yao, wakimkasirisha Bwana.
16 Naye atawatoa Israeli kwa ajili ya makosa ya Yeroboamu, aliyoyakosa, ambayo kwa hayo amewakosesha Israeli.
17 Basi mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda zake, akafika Tirza; naye alipofika kizingitini kwa nyumba, huyo kijana akafa.
18 Israeli wote wakamzika, wakamlilia; sawasawa na neno la Bwana, alilolinena kwa mkono wa mtumishi wake Ahiya nabii.
19 Na mambo yake Yeroboamu yaliyosalia, ya kupigana na ya kutawala, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli.
20 Na siku alizotawala Yeroboamu zilikuwa miaka ishirini na miwili; akalala na babaze, naye Nadabu mwanawe akatawala mahali pake.
21 Naye Rehoboamu mwana wa Sulemani akatawala katika Yuda. Rehoboamu akaanza kutawala alipokuwa mwenye miaka arobaini na mmoja, akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji aliouchagua Bwana miongoni mwa kabila zote za Israeli, ili aliweke jina lake huko. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni.
22 Basi Yuda wakafanya maovu machoni pa Bwana; wakamtia wivu, kwa makosa yao waliyoyakosa, kuliko yote waliyoyafanya baba zao.
23 Maana hao pia wakajijengea mahali pa juu, na nguzo, na maashera, juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi.
24 Na mahanithi walikuwako katika nchi, wakafanya sawasawa na machukizo yote ya mataifa Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.
25 Ikawa, mwaka wa tano wa mfalme Rehoboamu, akapanda Shishaki, mfalme wa Misri, juu ya Yerusalemu;
26 akazichukua hazina za nyumba ya Bwana, na hazina za nyumba ya mfalme; akazichukua zote. Akazichukua pia ngao zote za dhahabu alizozifanya Sulemani.
27 Mfalme Rehoboamu akafanya ngao za shaba mahali pake, akawakabidhi wakuu wa walinzi, waliongoja mlangoni pa nyumba ya mfalme.
28 Ikawa kila wakati mfalme alipoingia nyumbani mwa Bwana, hao walinzi walizichukua; wakazirudisha tena katika chumba cha walinzi.
29 Na mambo yake Rehoboamu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
30 Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu siku zote.
31 Rehoboamu akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni. Na mwanawe, Abiya, alitawala mahali pake.