0:00
0:00

Mlango 35

Naye Yosia akamfanyia Bwana pasaka huko Yerusalemu; wakachinja pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza.
2 Akawasimamisha makuhani katika malinzi yao, akawatia moyo kufanya utumishi wa nyumba ya Bwana.
3 Akawaambia Walawi, waliowafundisha Israeli wote, waliotakasika kwa Bwana, Wekeni sanduku takatifu katika nyumba aliyoijenga Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli; hamtakuwa tena na mzigo mabegani; sasa mtumikieni Bwana, Mungu wenu, na watu wake Israeli.
4 Mkajiweke tayari kwa kadiri ya nyumba za baba zenu, kwa zamu zenu, kama alivyoandika Daudi mfalme wa Israeli, na kama alivyoandika Sulemani mwanawe.
5 Mkasimame katika patakatifu, kama walivyogawanyika ndugu zenu, wana wa watu, kufuata nyumba za mababa, kadiri ya mgawanyiko wa kila nyumba ya baba, ya Walawi.
6 Mkachinje pasaka, mkajitakase, mkawatengenezee ndugu zenu, kutenda sawasawa na neno la Bwana kwa mkono wa Musa.
7 Tena Yosia akawapa wana wa watu, matoleo ya makundi, wana-kondoo na wana-mbuzi, yote yawe kwa ajili ya matoleo ya pasaka, wote waliokuwako, wakipata thelathini elfu, na ng'ombe elfu tatu; hao walitoka katika mali za mfalme.
8 Na wakuu wake wakawapa watu, na makuhani na Walawi matoleo ya hiari. Hilkia na wana na Yehieli, wakubwa wa nyumba ya Mungu, wakawapa makuhani, kuwa matoleo ya pasaka, wana-kondoo elfu mbili na mia sita, na ng'ombe mia tatu.
9 Konania naye, na Shemaya, na Nethaneli, ndugu zake, na Hashabia, na Yeieli, na Yozabadi, wakuu wa Walawi, wakawapa Walawi, kuwa matoleo ya pasaka, wana-kondoo elfu tano, na ng'ombe mia tano.
10 Hivyo huduma ikatengenezwa, wakasimama makuhani mahali pao, na Walawi kwa zamu zao, kama alivyoamuru mfalme.
11 Wakachinja pasaka, nao makuhani wakamimina damu waliyopokea mikononi mwao, Walawi wakachuna.
12 Wakaziondoa sadaka za kuteketezwa, wawape wana wa watu, kama walivyogawanyika kufuata nyumba za mababa, ili wamtolee Bwana, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Musa. Nao ng'ombe wakawafanya vivyo hivyo.
13 Wakaioka moto pasaka kama ilivyo sheria; wakatokosa matoleo matakatifu vyunguni, na masufuriani, na makaangoni, wakawachukulia upesi wana wa watu wote.
14 Baadaye wakajiandalia wenyewe, na makuhani; kwa sababu makuhani, wana wa Haruni, walikuwa na kazi ya kutoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta hata usiku; kwa hiyo Walawi wakajiandalia wenyewe, na makuhani, wana wa Haruni.
15 Nao waimbaji, wana wa Asafu wakasimama mahali pao, kama alivyoamuru Daudi, na Asafu, na Hemani, na Yeduthuni mwonaji wa mfalme; nao mabawabu walikuwa katika kila lango; hawakuhitaji kuondoka katika huduma yao, kwa kuwa ndugu zao Walawi wakawaandalia.
16 Basi huduma yote ya Bwana ikatengenezwa siku ile ile, kuifanya pasaka, na kutoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Bwana, kama alivyoamuru mfalme Yosia.
17 Wana wa Israeli waliokuwapo wakafanya pasaka wakati ule, na sikukuu ya mikate isiyochachwa muda wa siku saba.
18 Wala haikufanyika pasaka kama ile katika Israeli tangu siku za nabii Samweli; wala wafalme wa Israeli hawakufanya hata mmoja wao pasaka kama ile Yosia aliyoifanya, pamoja na makuhani, na Walawi, na Yuda wote na Israeli waliokuwapo, na wenyeji wa Yerusalemu.
19 Katika mwaka wa kumi na nane wa kutawala kwake Yosia ikafanyika pasaka hiyo.
20 Baada ya hayo yote, alipokwisha Yosia kulitengeneza hekalu, Neko, mfalme wa Misri, akakwea ili kupigana Karkemishi karibu na Frati; naye Yosia akatoka juu yake.
21 Lakini yeye akatuma kwake wajumbe, kusema, Ni nini niliyo nayo mimi na wewe, Ee mfalme wa Yuda? Sikuja juu yako leo, lakini juu ya nyumba niliyo na vita nayo; naye Mungu ameniamuru nifanye haraka; acha basi kumpinga Mungu, aliye pamoja nami, asikuharibu.
22 Walakini Yosia hakukubali kumgeuzia uso mbali, akajibadilisha apate kupigana naye, asiyasikilize maneno ya Neko, yaliyotoka kinywani kwa Mungu, akaja kupigana bondeni mwa Megido.
23 Nao wapiga upinde wakampiga Yosia; naye mfalme akawaambia watumishi wake, Niondoeni; kwani nimejeruhiwa sana.
24 Basi watumishi wake wakamtoa garini, wakamtia katika gari la pili alilokuwa nalo, wakamleta Yerusalemu; naye akafa, akazikwa makaburini mwa babaze. Wakamlilia Yosia Yuda wote na Yerusalemu.
25 Naye Yeremia akamlilia Yosia; na waimbaji wote waume kwa wake wakamtaja Yosia katika maombolezo yao, hata leo; hata wakayafanya kuwa ada kwa Israeli; nayo, tazama, yameandikwa katika maombolezo.
26 Basi mambo yote ya Yosia yaliyosalia, na matendo yake mema, sawasawa na yote yaliyoandikwa katika torati ya Bwana,
27 na mambo yake, ya kwanza na ya mwisho, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda.