0:00
0:00

Mlango 1

Basi Sulemani, mwana wa Daudi, alithibitishwa katika ufalme wake, naye Bwana, Mungu wake, alikuwa pamoja naye, akamtukuza mno.
2 Sulemani akasema na Israeli wote, na maakida wa maelfu, na wa mamia, na waamuzi, na kila shehe wa Israeli wote, wakuu wa nyumba za mababa.
3 Basi Sulemani akaenda mahali pa juu pa Gibeoni, na kusanyiko lote naye; kwani ndipo ilipokuwako hema ya kukutania ya Mungu, aliyoifanya Musa mtumishi wa Bwana jangwani.
4 Lakini sanduku la Mungu, Daudi alikuwa amelipandisha kutoka Kiriath-yearimu mpaka mahali Daudi alipolitengenezea; maana amelitandia hema katika Yerusalemu.
5 Tena madhabahu ya shaba, aliyoifanyiza Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, ilikuwako huko mbele ya maskani ya Bwana; Sulemani na kusanyiko wakaiendea.
6 Sulemani akaipandia huko madhabahu ya shaba mbele za Bwana, iliyokuwako hemani pa kukutania, akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu yake.
7 Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, Omba utakalo nikupe.
8 Sulemani akamwambia Mungu, Umemfanyia baba yangu Daudi fadhili kuu, nawe umenimilikisha mimi badala yake.
9 Basi sasa, Ee Bwana Mungu, na limyakinie baba yangu Daudi neno lako; maana umenitawaza niwe mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya nchi.
10 Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwahukumu watu wako hawa walio wengi?
11 Naye Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, wala hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha za wakuchukiao, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwahukumu watu wangu, niliokutawaza juu yao;
12 basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.
13 Akaja Sulemani kutoka mahali pa juu pa Gibeoni, toka mbele ya hema ya kukutania, mpaka Yerusalemu; akatawala juu ya Israeli.
14 Sulemani akakusanya magari na wapandao farasi; naye alikuwa na magari elfu na mia nne, na wapandao farasi kumi na mbili elfu, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu.
15 Mfalme akafanya fedha na dhahabu kuwa kama mawe humo Yerusalemu, na mierezi akaifanya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi.
16 Nao farasi, aliokuwa nao Sulemani wakaletwa toka Misri; wakapewa wafanya biashara wake mfalme kwa makundi; kila kundi na thamani yake.
17 Nao hupandisha, na kuleta kutoka Misri gari kwa shekeli mia sita za fedha, na farasi kwa mia na hamsini, vivyo watu wakawaletea wafalme wote wa Wahiti, na wafalme wa Shamu, mikononi mwao.