0:00
0:00

Mlango 26

Kwa zamu zao mabawabu; wa Wakora; Meshelemia mwana wa Kore, wa wana wa Ebiasafu.
2 Naye Meshelemia alikuwa na wana; Zekaria mzaliwa wa kwanza, Yediaeli wa pili, Zebadia wa tatu, Yathnieli wa nne;
3 Elamu wa tano, Yohana wa sita, Elioenai wa saba.
4 Naye Obed-edomu alikuwa na wana; Shemaya mzaliwa wa kwanza, Yehozabadi wa pili, Yoa wa tatu, na Sakari wa nne, na Nethaneli wa tano;
5 Amieli wa sita, Isakari wa saba, Peulethai wa nane; kwa jinsi Mungu alivyombariki.
6 Naye mwanawe Shemaya akazaliwa wana, waliomiliki juu ya mbari ya baba yao; kwa kuwa walikuwa waume mashujaa.
7 Wana wa Shemaya; Othni, na Refaeli, na Obedi, na Elzabadi, nduguze walikuwa mashujaa, Elihu, na Semakia.
8 Hao wote walikuwa wana wa Obed-edomu; wao na wana wao na ndugu zao, watu hodari wawezao huo utumishi; watu wa Obed-edomu sitini na wawili.
9 Naye Meshelemia alikuwa na wana na nduguze, watu mashujaa, kumi na wanane.
10 Hosa naye, wa wana wa Merari, alikuwa na wana; Shimri mkuu wao; (kwani ajapokuwa yeye si mzaliwa wa kwanza, babaye alimweka mkuu);
11 Hilkia wa pili, Tebalia wa tatu, Zekaria wa nne; wana wote wa Hosa pamoja na nduguze walikuwa watu kumi na watatu.
12 Katika hao zilikuwa zamu za mabawabu, yaani, katika hao wakuu, wenye ulinzi sawasawa na ndugu zao, wa kutumika katika nyumba ya Bwana.
13 Nao wakatupiwa kura kwa ajili ya kila lango, wadogo sawasawa na wakubwa, kwa kadiri ya mbari za baba zao.
14 Kura ya mashariki ya lango ikamwangukia Meshelemia. Ndipo wakamtupia kura Zekaria mwanawe, mshauri mwenye busara; na kura yake ikamtokea ya kaskazini.
15 Ya Obed-edomu ya kusini; na ya wanawe nyumba ya akiba.
16 Ya Shupimu na Hosa upande wa magharibi, langoni pa Shalekethi, hapo penye daraja ya kupandia, ulinzi kwa ulinzi.
17 Upande wa mashariki walikuwapo Walawi sita, kaskazini wanne kila siku, kusini wanne kila siku, na wa nyumba ya akiba wawili wawili.
18 Penye Parbari upande wa magharibi, walikuwapo wanne darajani, na wawili huko Parbari.
19 Hizo ndizo zamu za mabawabu; wa wana wa Wakora, na wa wana wa Merari.
20 Na katika Walawi; Ahia alikuwa juu ya hazina za nyumba ya Mungu, na juu ya hazina za vitu vilivyowekwa wakfu.
21 Wana wa Ladani; wana wa Wagershoni waliokuwa wa Ladani; wakuu wa mbari za mababa waliokuwa wa Ladani, Mgershoni; Yehieli.
22 Wana wa Yehieli; Zethamu, na Yoeli nduguye, juu ya hazina za nyumba ya Bwana.
23 Wa Waamramu, wa Waishari, wa Wahebroni, wa Wauzieli;
24 na Shebueli, mwana wa Gershomu, mwana wa Musa, alikuwa mtawala hazina zote.
25 Na nduguze; wa Eliezeri, Rehabia mwanawe, na Ishia mwanawe, na Yoramu mwanawe, na Zikri mwanawe, na Shelomothi mwanawe.
26 Huyo Shelomothi na ndugu zake walikuwa juu ya hazina zote za vitu vilivyowekwa wakfu, alivyoviweka wakfu mfalme Daudi, na hao wakuu wa mbari za mababa, na maakida wa maelfu na wa mamia, na maakida wa jeshi.
27 Katika nyara zilizopatikana vitani, waliweka wakfu sehemu, ili kuitengeneza nyumba ya Bwana.
28 Na vyote alivyoviweka wakfu Samweli mwonaji, na Sauli mwana wa Kishi, na Abneri mwana wa Neri, na Yoabu mwana wa Seruya; na mtu ye yote aliyekiweka wakfu kitu cho chote, kilikuwa chini ya mkono wa Shelomothi na nduguze.
29 Katika Waishari, Kenania na wanawe walikuwa kwa ajili ya kazi ya nje juu ya Israeli, kuwa maakida na makadhi.
30 Katika Wahebroni, Hashabia na nduguze, mashujaa, elfu na mia saba, walikuwa na usimamizi juu ya Israeli ng'ambo ya Yordani upande wa magharibi; kwa ajili ya kazi zote za Bwana, na kwa utumishi wa mfalme.
31 Katika Wahebroni Yeria alikuwa mkuu, yaani, wa hao Wahebroni kwa kufuata vizazi vyao kwa mbari za mababa. Katika mwaka arobaini wa kutawala kwake Daudi wakatafutwa, wakaonekana huko Yazeri ya Gileadi miongoni mwao waume mashujaa.
32 Na nduguze, mashujaa, walikuwa elfu mbili na mia saba, wakuu wa mbari za mababa, ambao mfalme Daudi aliwaweka wawe wasimamizi juu ya Wareubeni, na Wagadi, na nusu kabila ya Wamanase, kwa ajili ya kila neno lililomhusu Mungu, na kwa mambo ya mfalme.