1 Mambo ya Nyakati
Mlango 17
Ikawa, Daudi alipokuwa akikaa nyumbani mwake, Daudi akamwambia nabii Nathani, Angalia, mimi ninakaa katika nyumba ya mwerezi, bali sanduku la agano la Bwana linakaa chini ya mapazia.
2 Naye Nathani akamwambia Daudi, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; kwa maana Mungu yu pamoja nawe.
3 Ikawa usiku uo huo, neno la Mungu likamjia Nathani, kusema,
4 Nenda, kamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, Wewe hutanijengea nyumba ya kukaa;
5 kwa maana sikukaa ndani ya nyumba tangu siku ile nilipowaleta Israeli huku hata leo; lakini hema kwa hema nimehamia, na maskani kwa maskani.
6 Katika mahali mwote nilimokwenda na Israeli wote, je! Nimesema neno lo lote na mtu ye yote wa waamuzi wa Israeli, niliowaagiza kuwalisha watu wangu, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mwerezi?
7 Basi sasa ndivyo utakavyomwambia mtumishi wangu Daudi, Bwana wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo ili uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli;
8 nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina, kama jina la hao wakuu walioko duniani.
9 Tena nitawaagizia watu wangu Israeli mahali, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena kama hapo kwanza,
10 na tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi wawe juu ya watu wangu Israeli, nami nitawashinda adui zako wote. Pamoja na hayo nakuambia, ya kwamba Bwana atakujengea nyumba.
11 Hata itakuwa, siku zako zitakapotimia, uende na babazo, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayekuwa wa wana wako; nami nitaufanya imara ufalme wake.
12 Yeye ndiye atakayenijengea nyumba, nami nitakifanya imara kiti cha enzi cha ufalme wake milele.
13 Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; wala sitamwondolea fadhili zangu, kama nilivyomwondolea yeye aliyekuwa kabla yako;
14 ila nitamstarehesha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele; na kiti chake cha enzi kitathibitishwa milele.
15 Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi.
16 Ndipo akaingia Daudi mfalme, akaketi mbele za Bwana; akasema Mimi ni nani, Ee Bwana Mungu, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hata hapa?
17 Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Mungu; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumwa wako, kwa miaka mingi inayokuja, nawe umeniangalia sawasawa na hali ya mtu mwenye cheo, Ee Bwana Mungu.
18 Na Daudi akuambie nini tena zaidi kwa habari ya heshima aliyotendewa mtumwa wako? Kwa maana wewe umemjua mtumwa wako.
19 Ee Bwana, kwa ajili ya mtumwa wako, na kwa moyo wako mwenyewe, umeyatenda hayo makuu yote, ili yajulikane hayo matendo makuu yote.
20 Ee Bwana, hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu mwingine ila wewe, kwa kadiri tulivyosikia kwa masikio yetu.
21 Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake mwenyewe, ili wawe watu wake, na kujifanyia jina kwa njia ya mambo makuu, yenye kuogofya, kwa kufukuza mataifa mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri?
22 Kwa maana watu wako Israeli ndio uliowafanya kuwa watu wako wa milele; nawe, Bwana, umekuwa Mungu wao.
23 Basi sasa, Ee Bwana, neno lile ulilolinena katika habari za mtumwa wako, na katika habari za nyumba yake, na lifanywe imara milele, ukafanye kama ulivyosema.
24 Jina lako na liwe imara, likatukuzwe milele, kusema, Bwana wa majeshi ndiye Mungu wa Israeli, naam, Mungu juu ya Israeli; na hiyo nyumba ya Daudi mtumwa wako imefanywa imara mbele zako.
25 Kwa kuwa wewe, Ee Mungu wangu, umenifunulia mimi mtumwa wako ya kuwa utanijengea nyumba; kwa hiyo mimi mtumwa wako nimeona vema moyoni mwangu kuomba mbele yako.
26 Na sasa, Ee Bwana, wewe ndiwe Mungu, nawe umemwahidia mtumwa wako jambo hili jema;
27 nawe sasa umekuwa radhi kuibarikia nyumba ya mtumwa wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Bwana, umebarikia, nayo imebarikiwa milele.