0:00
0:00

Mlango 18

Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe.
2 Sauli akamtwaa siku ile, wala hakumwacha arudi tena nyumbani kwa baba yake.
3 Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe.
4 Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake.
5 Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; Sauli akamweka juu ya watu wa vita; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia.
6 Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda.
7 Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake.
8 Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme?
9 Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.
10 Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake.
11 Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili.
12 Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli.
13 Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe akida wake juu ya askari elfu; naye akatoka na kuingia mbele ya watu.
14 Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye Bwana alikuwa pamoja naye.
15 Sauli alipoona ya kwamba alitenda kwa busara sana, yeye alimwogopa.
16 Lakini Israeli wote na Yuda wakampenda Daudi; kwa kuwa alitoka na kuingia mbele yao.
17 Kisha Sauli akamwambia Daudi, Tazama, binti yangu mkubwa, Merabu, huyu nitakupa wewe ili umwoe; ila na wewe uniwie hodari wa vita, na kuvipiga vita vya Bwana. Maana Sauli alisema moyoni mwake, Mkono wangu usiwe juu yake, bali mkono wa Wafilisti na uwe juu yake.
18 Naye Daudi akamwambia Sauli, Mimi ni nani, na jamaa zangu ni akina nani, au mbari ya babangu, katika Israeli, hata mimi niwe mkwewe mfalme?
19 Lakini ikawa, wakati ule, ilipopasa Daudi apewe Merabu, binti Sauli, aliolewa na Adrieli, Mmeholathi.
20 Walakini Mikali, binti Sauli, alimpenda Daudi; watu wakamwambia Sauli, na neno hilo likampendeza.
21 Naye Sauli akasema moyoni, Mimi nitamwoza huyu, awe mtego kwake, tena kwamba mkono wa Wafilisti uwe juu yake. Basi Sauli akamwambia Daudi mara ya pili, Leo utakuwa mkwe wangu.
22 Naye Sauli akawaagiza watumishi wake, Zungumzeni na Daudi kwa siri, na kusema, Angalia, mfalme anakuridhia, na watumishi wake wote wanakupenda; haya basi! Na uwe mkwewe mfalme.
23 Nao watumishi wa Sauli wakanena maneno hayo masikioni mwa Daudi. Daudi akasema, Je! Ninyi mwaona kuwa ni shani mimi kuwa mkwewe mfalme, nami ni maskini, tena sina cheo?
24 Na hao watumishi wa Sauli wakampasha habari, wakisema, Ndivyo hivyo alivyosema Daudi.
25 Naye Sauli akasema, Mwambieni Daudi hivi, Mfalme hataki mahari yo yote, ila anataka govi mia za Wafilisti, ili ajilipize kisasi adui za mfalme. Basi Sauli alidhani kumwangamiza Daudi kwa mkono wa Wafilisti.
26 Na watumishi wake walipomwambia Daudi; maneno hayo, ilimpendeza Daudi sana kuwa mkwewe mfalme. Na siku zilikuwa hazijaisha bado;
27 basi Daudi akainuka, akaenda yeye na watu wake, akaua katika Wafilisti watu mia mbili; na Daudi akazileta govi zao, wakampa mfalme hesabu kamili, ili awe mkwewe mfalme. Naye Sauli akamwoza Mikali, binti yake.
28 Sauli akaona na kutambua ya kwamba Bwana alikuwa pamoja na Daudi; na huyo Mikali, binti Sauli, akampenda.
29 Naye Sauli akazidi kumwogopa Daudi; Sauli akawa adui yake Daudi sikuzote.
30 Wakati huo wakuu wa Wafilisti wakatoka; kisha ikawa, kila mara walipotoka, Daudi akatenda kwa busara zaidi ya watumishi wote wa Sauli hivyo jina lake likawa na sifa kuu.