1 Samweli
Mlango 11
Ikawa, kama baada ya mwezi mmoja, Nahashi, Mwamoni, akakwea na kupanga marago juu ya Yabesh-gileadi; na watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, Fanya mapatano nasi, na sisi tutakutumikia.
2 Huyo Nahashi, Mwamoni, akawaambia, Kwa sharti hii mimi nitapatana nanyi, kila mtu ang'olewe jicho la kuume; na kwa jambo hilo nitawashutumu Waisraeli wote pia.
3 Basi wazee wa Yabeshi wakamjibu, Tuachie siku saba, ili tutume wajumbe waende mipakani mwote mwa Israeli; kisha, ikiwa hakuna atakayetuokoa, tutakutokea.
4 Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote wakainua sauti zao wakalia.
5 Na tazama, Sauli akaja akifuata ng'ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi.
6 Na roho ya Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka sana.
7 Naye akatwaa jozi ya ng'ombe, akawakata-kata vipande, kisha akavipeleka vile vipande mipakani mwote mwa Israeli kwa mikono ya wajumbe, kusema, Ye yote asiyetoka nyuma ya Sauli na Samweli, ng'ombe zake watatendwa vivi hivi. Basi utisho wa Bwana ukawaangukia wale watu, wakatoka kama mtu mmoja.
8 Naye akawahesabu huko Bezeki; Waisraeli walikuwa mia tatu elfu, na Wayuda thelathini elfu.
9 Nao wakawaambia hao wajumbe waliokuja, Waambieni watu wa Yabesh-gileadi, Kesho, wakati wa jua kali, mtapata wokovu. Basi wale wajumbe wakaenda, wakawaarifu watu wa Yabeshi; nao walifurahiwa.
10 Kwa hiyo watu wa Yabeshi walisema, Kesho tutawatokea, nanyi mtatufanyia yote myaonayo kuwa ni mema.
11 Ikawa, kesho yake, Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu; nao wakaingia katikati ya marago kwenye zamu ya asubuhi, wakawapiga Waamoni hata wakati wa jua kali; kisha ikawa wale waliosalia wakatawanyika, hata wasiachwe wawili wao pamoja.
12 Ndipo watu walipomwambia Samweli, Ni nani yule aliyesema, Je! Huyo Sauli atatutawala? Walete watu hao, ili tuwaue.
13 Lakini Sauli akasema, Hakuna mtu atakayeuawa leo, maana leo Bwana amefanya wokovu katika Israeli.
14 Kisha Samweli akawaambia watu, Haya! Na twendeni mpaka Gilgali, ili tuuimarishe ufalme huko mara ya pili.
15 Nao watu wote wakaenda Gilgali; wakamtawaza Sauli mbele za Bwana huko Gilgali; wakachinja sadaka za amani mbele za Bwana; na huko Sauli na watu wote wa Israeli wakafurahi sana.