0:00
0:00

Mlango 3

Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao wakatoka Shitimu, wakafika mto wa Yordani, yeye na wana wa Israeli wote, wakakaa hapo kabla ya kuvuka.
2 Ikawa baada ya siku tatu, maakida wakapita katikati ya marago,
3 wakawaamuru watu wote wakisema, Mtakapoliona sanduku la agano la Bwana, Mungu wenu, na makuhani Walawi wakilichukua, ndipo mtakapoondoka hapa mlipo na kulifuata.
4 Lakini, na iwe nafasi kati ya ninyi na lile sanduku, kama dhiraa elfu mbili kiasi chake; msilikaribie mpate kuijua njia ambayo hamna budi kuiendea; kwa maana hamjapita njia hii bado.
5 Yoshua akawaambia watu, Jitakaseni; maana kesho Bwana atatenda mambo ya ajabu kati yenu.
6 Kisha Yoshua akawaambia makuhani, akasema, Liinueni sanduku la agano, mkavuke mbele ya hao watu. Wakaliinua sanduku la agano, wakatangulia mbele ya watu.
7 Bwana akamwambia Yoshua, Hivi leo nitaanza kukutukuza mbele ya Israeli wote, wapate kujua ya kuwa mimi nitakuwa pamoja na wewe, kama nilivyokuwa pamoja na Musa.
8 Nawe uwaamuru hao makuhani walichukuao sanduku la agano, ukawaambie, Mtakapofika ukingo wa maji ya Yordani, simameni katika Yordani.
9 Basi Yoshua akawaambia wana wa Israeli, Njoni huku, mkayasikie maneno ya Bwana, Mungu wenu.
10 Yoshua akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kuwa Mungu aliye hai yu kati yenu, na ya kuwa hatakosa kuwatoa mbele yenu Mkanaani, na Mhiti, na Mhivi, na Mperizi, na Mgirgashi, na Mwamori, na Myebusi.
11 Tazama, sanduku la agano la Bwana wa dunia yote linavuka mbele yenu na kuingia Yordani.
12 Basi sasa twaeni watu kumi na wawili katika kabila za Israeli, kila kabila mtu mmoja.
13 Itakuwa, wakati nyayo za makuhani walichukuao sanduku la Bwana, Bwana wa dunia yote, zitakaposimama katika maji ya Yordani, hayo maji ya Yordani yatatindika, maji yale yashukayo kutoka juu; nayo yatasimama kama chuguu.
14 Hata ikawa, hao watu walipotoka katika hema zao, ili kuvuka Yordani, makuhani waliolichukua sanduku la agano wakatangulia mbele ya watu,
15 basi hao waliolichukua hilo sanduku walipofika Yordani, na nyayo za makuhani waliolichukua sanduku zilipotiwa katika maji ya ukingoni, (maana Yordani hujaa hata kingo zake na kufurika wakati wote wa mavuno),
16 ndipo hayo maji yaliyoshuka kutoka juu yakasimama, yakainuka, yakawa chuguu, mbali sana, huko Adamu, mji ule ulio karibu na Sarethani, na maji yale yaliyotelemkia bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, yakatindika kabisa; watu wakavuka kukabili Yeriko.
17 Na hao makuhani waliolichukua sanduku la agano la Bwana wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Yordani; Israeli wote wakavuka katika nchi kavu, hata taifa lile lote likaisha kuvuka Yordani.