Yoshua
Mlango 14
Kisha hizi ndizo nchi ambazo wana wa Israeli walizitwaa katika nchi ya Kanaani, ambazo Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni, na vichwa vya nyumba za mababa wa kabila za Israeli, waliwagawanyia,
2 kwa kuandama hiyo kura ya urithi wao, vile vile kama Bwana alivyoamuru kwa mkono wa Musa, kwa ajili ya hizo kabila kenda, na hiyo nusu ya kabila.
3 Kwa kuwa Musa alikuwa amekwisha kuwapa urithi hizo kabila mbili na nusu, ng'ambo ya pili ya Yordani; lakini hakuwapa Walawi urithi uwao wote kati yao.
4 Kwa kuwa wana wa Yusufu walikuwa kabila mbili, Manase na Efraimu; nao hawakuwapa Walawi sehemu katika hiyo nchi, isipokuwa waliwapa miji wapate kuikaa, pamoja na viunga vyake kwa ajili ya wanyama wao wa mifugo, na kwa ajili ya riziki zao.
5 Vile vile kama Bwana alivyomwamuru Musa, hao wana wa Israeli walifanya vivyo, nao wakaigawanya hiyo nchi.
6 Wakati huo wana wa Yuda walimkaribia Yoshua hapo Gilgali; na Kalebu, mwana wa Yefune, huyo Mkenizi, akamwambia, Wewe wajua hilo neno Bwana alilomwambia Musa, huyo mtu wa Mungu, katika habari zangu, na katika habari zako wewe, tulipokuwa katika Kadesh-barnea.
7 Mimi nilikuwa mtu wa miaka arobaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa Bwana aliponituma niende kutoka Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu.
8 Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliiyeyusha mioyo ya watu; ila mimi nilimfuata Bwana, Mungu wangu, kwa utimilifu.
9 Kisha Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu wewe umemfuata Bwana, Mungu wako, kwa utimilifu.
10 Sasa basi, angalia, yeye Bwana ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arobaini na mitano, tangu wakati huo Bwana alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli waliokuwa wakienenda barani; na sasa tazama, hivi leo nimepata miaka themanini na mitano umri wangu.
11 Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani.
12 Basi sasa unipe mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama Bwana alivyonena.
13 Yoshua akambarikia, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake.
14 Kwa hiyo Hebroni ukawa urithi wa Kalebu, mwana wa Yefune, Mkenizi, hata leo; kwa sababu alimwandama Bwana, Mungu wa Israeli, kwa utimilifu.
15 Basi jina la Hebroni hapo kwanza uliitwa Kiriath-arba; huyo Arba alikuwa ni mtu mkubwa kupita wenziwe wote katika hao Waanaki. Hiyo nchi nayo ikatulia, vita vikakoma.