0:00
0:00

Mlango 49

Yakobo akawaita wanawe, akasema, Kusanyikeni, ili niwaambie yatakayowapata siku za mwisho.
2 Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo, Msikilizeni Israeli, baba yenu.
3 Reubeni, u mzaliwa wangu wa kwanza, Nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu. Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu.
4 Umeruka mpaka kama maji, basi usiwe na ukuu, Kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba yako, Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu.
5 Simeoni na Lawi ni ndugu; Panga zao ni silaha za jeuri.
6 Nafsi yangu, usiingie katika siri yao, Fahari yangu usiungane na kusanyiko lao, Maana katika ghadhabu yao walimuua mtu, Na kwa ukaidi wao walikata mshipa wa ng'ombe;
7 Ghadhabu yao na ilaaniwe, maana ilikuwa kali, Na hasira yao, maana ilikuwa haina huruma. Nitawagawa katika Yakobo, Nitawatawanya katika Israeli.
8 Yuda, ndugu zako watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia.
9 Yuda ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakaye mwamsha?
10 Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.
11 Atafunga punda wake katika mzabibu, Na mwana-punda wake katika mzabibu mzuri. Amefua nguo zake kwa mvinyo, Na mavazi yake kwa damu ya zabibu.
12 Macho yake yatakuwa mekundu kwa mvinyo, Na meno yake yatakuwa meupe kwa maziwa.
13 Zabuloni atakaa pwani ya bahari, Naye atakuwa kama pwani za kuegesha merikebu, Na mpaka wake utakuwa kando ya Sidoni.
14 Isakari ni punda hodari, Ajilazaye kati ya mazizi ya kondoo;
15 Akaona mahali pa raha, kuwa pema, Na nchi, ya kuwa ni nzuri, Akainama bega lake lichukue mizigo, Akawa mtumishi kwa kazi ngumu.
16 Dani atahukumu watu wake, Kama moja ya makabila ya Israeli;
17 Dani atakuwa nyoka barabarani, Bafe katika njia, Aumaye visigino vya farasi, Hata apandaye ataanguka chali.
18 Wokovu wako nimeungoja, Ee Bwana.
19 Gadi, jeshi litamsonga, Lakini atawasonga wao mpaka visigino.
20 Asheri, chakula chake kitakuwa kinono, Naye atatoa tunu za kifalme.
21 Naftali ni ayala aliyefunguliwa; Anatoa maneno mazuri.
22 Yusufu ni mti mchanga wenye kuzaa, Mti mchanga wenye kuzaa karibu na chemchemi, Matwi yake yametanda ukutani.
23 Wapiga mishale walimtenda machungu, Wakamtupia, wakamwudhi,
24 Lakini upinde wake ukakaa imara, Mikono yake ikapata nguvu, Kwa mikono ya Mwenye Enzi wa Yakobo; Kwa jina la mchungaji, yeye jiwe la Israeli,
25 Naam, kwa Mungu wa baba yako atakaye kusaidia; Kwa mibaraka ya mbinguni juu. Mibaraka ya vilindi vilivyo chini, Mibaraka ya maziwa, na ya mimba.
26 Mibaraka ya baba yako Imepita mibaraka ya milima ya kale, Vitu vinavyotamanika vya vilima vya milele; Na vikae juu ya kichwa cha Yusufu, Juu ya utosi wa kichwa chake aliye mkuu kati ya ndugu zake.
27 Benyamini ni mbwa-mwitu mwenye kurarua-rarua Asubuhi atakula mawindo, Na jioni atagawanya mateka.
28 Hizo zote ndizo kabila za Israeli kumi na mbili. Na hayo ndiyo aliyowaambia baba yao, na kuwabariki; mmoja mmoja kwa mbaraka wake aliwabariki.
29 Akawaamuru, akasema, Mimi ninakwenda kukusanywa pamoja na watu wangu; mnizike pamoja na baba zangu, katika pango iliyomo shambani mwa Efroni, Mhiti;
30 katika ile pango iliyomo shambani mwa Makpela, iliyo mbele ya Mamre katika nchi ya Kanaani, aliyoinunua Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake ya kuzikia.
31 Humo walimzika Ibrahimu, na Sara mkewe; humo wakamzika Isaka, na Rebeka mkewe; nami humo nikamzika Lea;
32 shamba na pango iliyomo lililonunuliwa kwa wazawa wa Hethi.
33 Basi Yakobo alipokwisha kuwaagiza wanawe, akakunja miguu yake kitandani, akafa, akakusanywa pamoja na watu wake.