0:00
0:00

Mlango 22

Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa.
2 Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.
3 Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu.
4 Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho yake, akapaona mahali pakali mbali.
5 Ibrahimu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na kuwarudia tena.
6 Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja.
7 Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa?
8 Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja.
9 Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni.
10 Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe.
11 Ndipo malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa.
12 Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee.
13 Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.
14 Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire,kama watu wasemavyo hata leo,Katika mlima wa BWANA itapatikana.
15 Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni
16 akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,
17 katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao;
18 na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.
19 Basi Ibrahimu akawarudia vijana wake, wakaondoka, wakaenda zao pamoja mpaka Beer-sheba; Ibrahimu akakaa huko Beer-sheba.
20 Ikawa baada ya mambo hayo, Ibrahimu akaambiwa ya kwamba, Tazama, Milka naye amemzalia Nahori ndugu yako wana;
21 Usi, mzaliwa wa kwanza wake, na Buzi nduguye, na Kemueli, baba wa Aramu;
22 na Kesedi, na Hazo, na Pildashi, na Yidlafu, na Bethueli.
23 Bethueli akamzaa Rebeka; hao wanane Milka alimzalia Nahori ndugu wa Ibrahimu.
24 Na suria wake Reuma naye alizaa Teba na Gahamu na Tahashi na Maaka.