Mwanzo
Mlango 27
Ikawa Isaka alipokuwa mzee, na macho yake yamepofuka asione, akamwita Esau, mwanawe mkubwa, akamwambia, Mwanangu. Naye akamwitikia, Mimi hapa.
2 Akasema, Tazama, sasa mimi nimekuwa mzee, wala sijui siku ya kufa kwangu.
3 Basi, nakuomba, chukua mata yako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie mawindo;
4 ukanifanyie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki, kabla sijafa.
5 Na Rebeka akasikia, Isaka aliposema na Esau mwanawe. Basi Esau akaenda nyikani awinde mawindo, ayalete.
6 Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, akisema, Angalia, nimemsikia baba yako akisema na Esau, ndugu yako, akinena,
7 Niletee mawindo, ukanifanyie chakula kitamu ili nile, na kukubariki mbele za Bwana kabla ya kufa kwangu.
8 Basi, mwanangu, sikiliza sauti yangu kama nitakavyokuagiza.
9 Enenda sasa kundini ukanitwalie wana-mbuzi wawili walio wema, nami nitawafanya chakula kitamu kwa baba yako, namna ile aipendayo.
10 Kisha utampelekea baba yako, apate kula, ili akubariki kabla ya kufa kwake.
11 Yakobo akamwambia Rebeka mamaye, Esau ndugu yangu ni mtu mwenye malaika, na mimi ni mtu laini.
12 Labda baba yangu atanipapasa, nami nitakuwa machoni pake kama mdanganyifu; nami nitaleta juu yangu laana wala si mbaraka.
13 Mamaye akamwambia, Laana yako na iwe juu yangu, mwanangu, usikie sauti yangu tu, enenda ukaniletee wana-mbuzi.
14 Akaenda, akawatwaa, akamletea mamaye. Mamaye akafanya chakula kitamu namna ile aliyopenda babaye.
15 Kisha Rebeka akatwaa mavazi mazuri ya Esau mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo.
16 Na ngozi za wana-mbuzi akamvika mikononi, na katika ulaini wa shingo yake.
17 Naye akampa Yakobo mwanawe mikononi mwake hicho chakula kitamu, na mkate alioufanya.
18 Akaja kwa baba yake, akasema, Babangu. Akasema, Mimi hapa, U nani wewe, mwanangu?
19 Yakobo akamwambia babaye, Mimi ni Esau, mzaliwa wako wa kwanza, nimefanya kama ulivyoniambia. Ondoka, tafadhali, ukae kitako, ule mawindo yangu, ili roho yako inibariki.
20 Isaka akamwuliza mwanawe, Imekuwaje umepata upesi namna hii, mwanangu? Akasema, Kwa sababu Bwana, Mungu wako, amenifanikisha.
21 Isaka akamwambia Yakobo, Karibu, tafadhali, ili nikupapase, mwanangu, nione kwamba wewe ndiwe mwanangu Esau, ama siyo.
22 Basi Yakobo akamkaribia Isaka, babaye, naye akampapasa, akasema, Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau.
23 Wala hakumtambua, kwa maana mikono yake ilikuwa kama mikono ya Esau, ndugu yake, yenye malaika; basi akambariki.
24 Akamwuliza, Wewe ndiwe kweli mwanangu Esau? Akasema, Ndimi.
25 Akasema, Niletee karibu nami nipate kula mawindo ya mwanangu, ili roho yangu ikubariki. Akamsogezea karibu, naye akala; kisha akamletea mvinyo, akanywa.
26 Isaka, baba yake, akamwambia, Njoo karibu sasa, ukanibusu, mwanangu.
27 Akakaribia akambusu. Naye akasikia harufu ya mavazi yake, akambariki akasema, Tazama, harufu ya mwanangu Ni kama harufu ya shamba alilolibariki Bwana.
28 Mungu na akupe ya umande wa mbingu, Na ya manono ya nchi, Na wingi wa nafaka na mvinyo.
29 Mataifa na wakutumikie Na makabila wakusujudie, Uwe bwana wa ndugu zako, Na wana wa mama yako na wakusujudie. Atakayekulaani alaaniwe, Na atakayekubariki abarikiwe.
30 Ikawa Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, na alipokuwa Yakobo ndiyo kwanza ametoka mbele ya Isaka, baba yake, mara Esau ndugu yake akaja kutoka katika kuwinda kwake.
31 Naye pia amefanya chakula kitamu akamletea babaye, akamwambia baba yake. Babangu na aondoke, ale mawindo ya mwanawe, ili roho yako inibariki.
32 Isaka, baba yake, akamwuliza, U nani wewe? Akasema, Mimi ni mwanao, Esau, mzaliwa wako wa kwanza.
33 Isaka akatetemeka tetemeko kuu sana, akasema, Ni nani basi yule aliyetwaa mawindo akaniletea? Nami nimekwisha kula kabla hujaja wewe, nikambariki; naam, naye atabarikiwa.
34 Esau aliposikia maneno ya babaye, akalia kilio kikubwa cha uchungu sana, akamwambia babaye, Nibariki na mimi, mimi nami, Ee babangu.
35 Akasema, Nduguyo amekuja kwa hila, akauchukua mbaraka wako.
36 Akasema, Je! Hakuitwa Yakobo kwa haki, maana amejitia mahali pangu mara mbili hizi? Alichukua haki yangu ya mzaliwa wa kwanza, na sasa amechukua mbaraka wangu. Akasema, Je! Hukuniwekea na mimi mbaraka?
37 Isaka akajibu, akamwambia Esau, Tazama, nimemfanya awe bwana wako, na ndugu zake wote nimempa kuwa watumishi wake; kwa nafaka na mvinyo nimemtegemeza, nami nikufanyie nini sasa, mwanangu?
38 Esau akamwambia babaye, Una mbaraka mmoja tu, babangu? Unibariki mimi, mimi nami, Ee babangu. Esau akapaza sauti yake, akalia.
39 Isaka, baba yake, akajibu, akamwambia,Angalia,penye manono ya nchi patakuwa makao yako,Na penye umande wa mbingu unaotoka juu.
40 Kwa upanga wako wewe utaishi, nawe utamtumikia nduguyo; Na itakuwa utakapoponyoka, Utalivunja kongwa lake katika shingo yako.
41 Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo.
42 Rebeka akaarifiwa maneno ya Esau, mwanawe mkubwa. Akapeleka mtu kumwita Yakobo, mwanawe mdogo, akamwambia, Tazama, katika habari zako Esau, ndugu yako, anajifariji moyo wake, maana anakusudia kukuua.
43 Na sasa, mwanangu, sikia sauti yangu, uondoke, ukimbilie kwa Labani, ndugu yangu huko Harani;
44 ukae kwake siku chache, hata ghadhabu ya ndugu yako igeuke;
45 hata ikuondokee ghadhabu ya ndugu yako, akasahau uliyomtenda. Ndipo nitakapopeleka watu kukuchukua kutoka huko. Kwa nini nifiwe nanyi nyote wawili siku moja?
46 Rebeka akamwambia Isaka, Rohoni mwangu sina raha kwa sababu ya hao binti za Hethi. Kama Yakobo akitwaa mke katika binti za Hethi, kama hawa binti za nchi, maisha yangu yatanifaidia nini?