0:00
0:00

Mlango 22

Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung'aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo,
2 katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.
3 Wala hapatakuwa na laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia;
4 nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao.
5 Wala hapatakuwa na usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu huwatia nuru, nao watatawala hata milele na milele.
6 Kisha akaniambia, Maneno haya ni amini na kweli. Naye Bwana, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumwa wake mambo ambayo hayana budi kuwako upesi.
7 Na tazama, naja upesi; heri yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.
8 Nami Yohana ndimi niliyeyasikia na kuyaona mambo hayo. Na hapo nilipoyasikia na kuyaona nalianguka, ili nisujudu mbele ya miguu ya malaika yule mwenye kunionyesha hayo.
9 Naye akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako, na wa ndugu zako manabii, na wa wale wayashikao maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu.
10 Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.
11 Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa.
12 Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.
13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.
14 Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake.
15 Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya.
16 Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung'aa ya asubuhi.
17 Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure.
18 Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
19 Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.
20 Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu.
21 Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote. Amina.