Ufunuo wa Yohana
Mlango 20
Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake.
2 Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu;
3 akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache.
4 Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu.
5 Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu.
6 Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu.
7 Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake;
8 naye atatoka kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari.
9 Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa. Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala.
10 Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.
11 Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana.
12 Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.
13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
14 Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.
15 Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.