0:00
0:00

Mlango 7

Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki;
2 ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani;
3 hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele.
4 Basi, angalieni jinsi mtu huyo alivyokuwa mkuu, ambaye Ibrahimu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara.
5 Na katika wana wa Lawi nao, wale waupatao ukuhani, wana amri kutwaa sehemu ya kumi kwa watu wao, yaani, ndugu zao, kwa agizo la sheria, ijapokuwa wametoka katika viuno vya Ibrahimu.
6 Bali yeye, ambaye uzazi wake haukuhesabiwa kuwa umetoka kwa hao, alitwaa sehemu ya kumi kwa Ibrahimu, akambariki yeye aliye na ile ahadi.
7 Wala haikanushiki kabisa kwamba mdogo hubarikiwa na mkubwa.
8 Na hapa wanadamu wapatikanao na kufa hutwaa sehemu ya kumi; bali huko yeye ashuhudiwaye kwamba yu hai.
9 Tena yaweza kusemwa ya kuwa, kwa njia ya Ibrahimu, hata Lawi apokeaye sehemu ya kumi alitoa sehemu ya kumi;
10 kwa maana alikuwa katika viuno vya baba yake, hapo Melkizedeki alipokutana naye.
11 Basi, kama ukamilifu ulikuwapo kwa ukuhani wa Lawi; (maana watu wale waliipata sheria kwa huo); kulikuwa na haja gani tena ya kuhani mwingine ainuke, kwa mfano wa Melkizedeki, wala asihesabiwe kwa mfano wa Haruni?
12 Maana ukuhani ule ukibadilika, hapana budi sheria nayo ibadilike.
13 Maana yeye aliyenenwa hayo alikuwa mshirika wa kabila nyingine, ambayo hapana mtu wa kabila hiyo aliyeihudumia madhabahu.
14 Maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika Yuda, kabila ambayo Musa hakunena neno lo lote juu yake katika mambo ya ukuhani.
15 Tena hayo tusemayo ni dhahiri sana zaidi, ikiwa ametokea kuhani mwingine mithili ya Melkizedeki;
16 asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa nguvu za uzima usio na ukomo;
17 maana ameshuhudiwa kwamba, Wewe u kuhani milele Kwa mfano wa Melkizedeki.
18 Maana, kuna kubatiliwa kwa ile amri iliyotangulia, kwa sababu ya udhaifu wake, na kutokufaa kwake;
19 (kwa maana ile sheria haikukamilisha neno); na pamoja na hayo kuliingizwa matumaini yaliyo mazuri zaidi, ambayo kwa hayo twamkaribia Mungu.
20 Na kwa kuwa haikuwa pasipo kiapo,
21 (maana wale walifanywa makuhani pasipo kiapo; bali yeye, pamoja na kiapo, kwa yeye aliyemwambia, Bwana ameapa wala hataghairi, Wewe u kuhani wa milele;)
22 basi kwa kadiri hii Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi.
23 Tena wale walifanywa makuhani wengi, kwa sababu wazuiliwa na mauti wasikae;
24 bali yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka.
25 Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee.
26 Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu;
27 ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake.
28 Maana torati yawaweka wanadamu walio na unyonge kuwa makuhani wakuu; bali hilo neno la kiapo kilichokuja baada ya torati limemweka Mwana, aliyekamilika hata milele.