Waebrania
Mlango 4
Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa.
2 Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliosikia.
3 Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile; kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu:
4 Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote;
5 na hapa napo, Hawataingia rahani mwangu.
6 Basi, kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao,
7 aweka tena siku fulani, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo; kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu.
8 Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingaliinena siku nyingine baadaye.
9 Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu.
10 Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake.
11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi.
12 Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
13 Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.
14 Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu.
15 Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.
16 Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.