0:00
0:00

Mlango 19

Basi ndipo Pilato alipomtwaa Yesu, akampiga mijeledi.
2 Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau.
3 Wakawa wakimwendea, wakisema, Salamu! Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga makofi.
4 Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia, Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yo yote kwake.
5 Ndipo Yesu alipotoka nje, naye amevaa ile taji ya miiba, na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, Tazama, mtu huyu!
6 Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema, Msulibishe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake.
7 Wayahudi wakamjibu, Sisi tunayo sheria, na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.
8 Basi Pilato aliposikia neno hilo, akazidi kuogopa.
9 Akaingia tena ndani ya ile Praitorio, akamwambia Yesu, Wewe umetokapi? Lakini Yesu hakumpa jibu lo lote.
10 Basi Pilato akamwambia, Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulibisha?
11 Yesu akamjibu, Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu; kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.
12 Na tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua; lakini Wayahudi wakapiga makelele wakisema, Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari.
13 Basi Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha.
14 Nayo ilikuwa Maandalio ya pasaka, yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi, Tazama, Mfalme wenu!
15 Basi wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Je! Nimsulibishe mfalme wenu! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.
16 Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu.
17 Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha.
18 Wakamsulibisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati.
19 Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI.
20 Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale aliposulibiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa Kiebrania, na Kirumi, na Kiyunani.
21 Basi wakuu wa makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato, Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi.
22 Pilato akajibu, Niliyoandika nimeyaandika.
23 Nao askari walipomsulibisha Yesu, waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu.
24 Basi wakaambiana, Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani. Ili litimie andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, Na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari.
25 Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene.
26 Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao.
27 Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.
28 Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu.
29 Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani.
30 Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.
31 Basi Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe.
32 Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja naye.
33 Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu;
34 lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji.
35 Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki.
36 Kwa maana hayo yalitukia ili andiko litimie, Hapana mfupa wake utakaovunjwa.
37 Na tena andiko lingine lanena, Watamtazama yeye waliyemchoma.
38 Hata baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu, (lakini kwa siri, kwa hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akauondoa mwili wake.
39 Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta machanganyiko ya manemane na uudi, yapata ratli mia.
40 Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika.
41 Na pale pale aliposulibiwa palikuwa na bustani; na ndani ya bustani mna kaburi jipya, ambalo hajatiwa bado mtu ye yote ndani yake.
42 Humo basi, kwa sababu ya Maandalio ya Wayahudi, wakamweka Yesu; maana lile kaburi lilikuwa karibu.