0:00
0:00

Mlango 11

Basi mtu mmoja alikuwa hawezi, Lazaro wa Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake.
2 Ndiye Mariamu yule aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye alikuwa hawezi.
3 Basi wale maumbu wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye umpendaye hawezi.
4 Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo.
5 Naye Yesu alimpenda Martha na umbu lake na Lazaro.
6 Basi aliposikia ya kwamba hawezi, alikaa bado siku mbili pale pale alipokuwapo.
7 Kisha, baada ya hayo, akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Uyahudi tena.
8 Wale wanafunzi wakamwambia, Rabi, juzijuzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe unakwenda huko tena?
9 Yesu akajibu, Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu.
10 Bali akienda usiku hujikwaa; kwa sababu nuru haimo ndani yake.
11 Aliyasema hayo; kisha, baada ya hayo, akawaambia, Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha.
12 Basi wale wanafunzi wakamwambia, Bwana, ikiwa amelala, atapona.
13 Lakini Yesu alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena habari ya kulala usingizi.
14 Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amekufa.
15 Nami nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini; lakini na twendeni kwake.
16 Basi Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye.
17 Basi Yesu alipofika, alimkuta amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne.
18 Na Bethania ilikuwa karibu na Yerusalemu, kadiri ya maili mbili hivi;
19 na watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari ya ndugu yao.
20 Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani.
21 Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa.
22 Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa.
23 Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka.
24 Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho.
25 Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;
26 naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?
27 Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.
28 Naye alipokwisha kusema hayo, alikwenda zake; akamwita umbu lake Mariamu faraghani, akisema, Mwalimu yupo anakuita.
29 Naye aliposikia, aliondoka upesi, akamwendea.
30 Na Yesu alikuwa hajafika ndani ya kijiji; lakini alikuwa akalipo pale pale alipomlaki Martha.
31 Basi wale Wayahudi waliokuwapo na Mariamu nyumbani, wakimfariji, walipomwona jinsi alivyoondoka upesi na kutoka, walimfuata; huku wakidhania ya kuwa anakwenda kaburini ili alie huko.
32 Basi Mariamu alipofika pale alipokuwapo Yesu, na kumwona, alianguka miguuni pake, akamwambia, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa.
33 Basi Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliofuatana naye wanalia, aliugua rohoni, akafadhaika roho yake,
34 akasema, Mmemweka wapi? Wakamwambia, Bwana, njoo utazame.
35 Yesu akalia machozi.
36 Basi Wayahudi wakasema, Angalieni jinsi alivyompenda.
37 Bali wengine wao wakasema, Je! Huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?
38 Basi Yesu, hali akiugua tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo lilikuwa ni pango, na jiwe limewekwa juu yake.
39 Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne.
40 Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu?
41 Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia.
42 Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma.
43 Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje.
44 Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.
45 Basi wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Mariamu, na kuyaona yale aliyoyafanya, wakamwamini.
46 Lakini wengine wakaenda zao kwa Mafarisayo, wakawaambia aliyoyafanya Yesu.
47 Basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakakusanya baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu afanya ishara nyingi.
48 Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja, watatuondolea mahali petu na taifa letu.
49 Mtu mmoja miongoni mwao, Kayafa, aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, akawaambia, Ninyi hamjui neno lo lote;
50 wala hamfikiri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima.
51 Na neno hilo yeye hakulisema kwa nafsi yake; bali kwa kuwa alikuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, alitabiri ya kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa hilo.
52 Wala si kwa ajili ya taifa hilo tu; lakini pamoja na hayo awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika, ili wawe wamoja.
53 Basi tangu siku ile walifanya shauri la kumwua.
54 Kwa hiyo Yesu hakutembea tena kwa wazi katikati ya Wayahudi; bali alitoka huko, akaenda mahali karibu na jangwa, mpaka mji uitwao Efraimu; akakaa huko pamoja na wanafunzi wake.
55 Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; na wengi wakakwea toka mashambani kwenda Yerusalemu kabla ya Pasaka, ili wajitakase.
56 Basi wao wakamtafuta Yesu, wakasemezana hali wamesimama hekaluni, Mwaonaje? Haji kabisa sikukuu hii?
57 Na wakuu wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri ya kwamba mtu akimjua alipo, alete habari, ili wapate kumkamata.