Mambo ya Walawi
Mlango 23
Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Sikukuu za Bwana, ambazo mtazipigia mbiu kuwa ni makusanyiko matakatifu; hizi ni sikukuu zangu.
3 Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yo yote; ni Sabato kwa Bwana katika makao yenu yote.
4 Sikukuu za Bwana ni hizi, ni makusanyiko matakatifu, ambayo mtayapigia mbiu kwa nyakati zake.
5 Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni pasaka ya Bwana.
6 Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa Bwana ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba.
7 Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu msifanye kazi yo yote ya utumishi.
8 Lakini mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.
9 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
10 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapokuwa mmekwisha ingia hiyo nchi niwapayo, na kuyavuna mavuno yake, ndipo mtakapomletea kuhani mganda wa malimbuko ya mavuno yenu;
11 naye atautikisa mganda mbele za Bwana ili kwamba ukubaliwe kwa ajili yenu; siku ya pili baada ya Sabato kuhani atautikisa.
12 Na siku hiyo mtakayoutikisa mganda, mtamsongeza mwana-kondoo wa kiume mkamilifu wa mwaka wa kwanza awe sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana.
13 Na sadaka yake ya unga itakuwa sehemu za kumi mbili za efa za unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, ni kafara iliyosongezwa kwa Bwana kwa moto kuwa harufu ya kupendeza; na sadaka yake ya kinywaji itakuwa ni divai, robo ya hini.
14 Nanyi msile mkate, wala bisi, wala masuke machanga, hata siku iyo hiyo, hata mtakapokuwa mmekwisha kuleta sadaka ya Mungu wenu; hii ni amri ya milele katika vizazi vyenu katika makao yenu yote.
15 Nanyi mtajihesabia tangu siku ya pili baada ya Sabato, tangu siku hiyo mliyouleta mganda wa sadaka ya kutikiswa; zitatimia Sabato saba;
16 hata siku ya pili ya hiyo Sabato ya saba mtahesabu siku hamsini; nanyi mtamsongezea Bwana sadaka ya unga mpya.
17 Mtatoa katika makao yenu mikate miwili ya kutikiswa, itakuwa ya sehemu za kumi mbili za efa; itakuwa ya unga mwembamba, itaokwa na chachu, iwe malimbuko kwa Bwana.
18 Nanyi, pamoja na hiyo mikate, mtasongeza wana-kondoo saba, walio wakamilifu, wa mwaka wa kwanza, na ng'ombe mume mmoja, na kondoo waume wawili; watakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana, pamoja na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji, sadaka ya harufu ya kupendeza iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.
19 Nanyi mtasongeza mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili waume wa mwaka wa kwanza kuwa dhabihu ya sadaka za amani.
20 Kisha kuhani atawatikisa pamoja na hiyo mikate ya malimbuko kuwa sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana, pamoja na wale wana-kondoo wawili; watakuwa watakatifu kwa Bwana, wawe wa huyo kuhani.
21 Nanyi mtapiga mbiu siku iyo hiyo; kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; msifanye kazi yo yote ya utumishi; ni amri ya milele katika makao yenu yote, katika vizazi vyenu.
22 Nanyi hapo mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala msiyakusanye masazo ya mavuno yako; utayaacha kwa ajili ya huyo maskini, na mgeni; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
23 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
24 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi, kutakuwa na kustarehe kabisa kwenu, ni ukumbusho wa kuzipiga baragumu, ni kusanyiko takatifu.
25 Msifanye kazi yo yote ya utumishi; nanyi mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto.
26 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
27 Lakini siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ni siku ya upatanisho; itakuwa kusanyiko takatifu kwenu, nanyi mtazitesa nafsi zenu; nanyi mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto.
28 Nanyi msifanye kazi yo yote siku hiyo; kwa kuwa ni siku ya upatanisho, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu mbele za Bwana, Mungu wenu.
29 Kwa kuwa mtu awaye yote asiyejitesa mwenyewe siku iyo hiyo, atakatiliwa mbali na watu wake.
30 Na mtu ye yote afanyaye kazi ya namna yo yote siku hiyo, mtu huyo nitamwangamiza atoke katika watu wake.
31 Msifanye kazi ya namna yo yote; ni amri ya milele katika vizazi vyenu, katika makao yenu yote.
32 Itakuwa kwenu sabato ya kustarehe kabisa, nanyi mtazitesa nafsi zenu; siku ya kenda ya mwezi wakati wa jioni, tangu jioni hata jioni, mtaishika hiyo Sabato yenu.
33 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
34 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa saba ni sikukuu ya vibanda muda wa siku saba kwa Bwana.
35 Siku ya kwanza kutakuwa na kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.
36 Mtamsongezea Bwana sadaka kwa moto siku saba; siku ya nane kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; nanyi mtamsongezea Bwana sadaka kwa moto; ni mkutano wa makini huu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.
37 Sikukuu za Bwana ni hizi, ambazo mtazipigia mbiu ya kuwa ni makusanyiko matakatifu, ili mmsongezee Bwana sadaka kwa moto, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na dhabihu, na sadaka za kinywaji, kila sadaka kwa siku yake;
38 zaidi ya hizo Sabato za Bwana, na zaidi ya matoleo yenu, na zaidi ya hizo nadhiri zenu zote, na zaidi ya sadaka zenu za hiari, ambazo mwampa Bwana.
39 Lakini siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, hapo mtakapokuwa mmekwisha kuyachuma mavuno ya nchi, mtaweka sikukuu ya Bwana muda wa siku saba; siku ya kwanza kutakuwa na kustarehe kabisa, na siku ya nane kutakuwa na kustarehe kabisa.
40 Nanyi siku ya kwanza mtajipatia matunda ya miti mizuri, na makuti ya mitende, na matawi ya miti minene, na mierebi ya vijitoni; nanyi mtafurahi mbele za Bwana, Mungu wenu, muda wa siku saba.
41 Nanyi mtaishika kuwa sikukuu kwa Bwana muda wa siku saba katika mwaka; ni amri ya milele katika vizazi vyenu; mtaishika katika mwezi wa saba.
42 Mtakaa katika vibanda muda wa siku saba; wazalia wote wa Israeli watakaa katika vibanda;
43 ili vizazi vyenu vipate kujua ya kuwa niliwaketisha wana wa Israeli katika vibanda, hapo nilipowaleta kutoka nchi ya Misri; mimi ndimi Bwana Mungu wenu.
44 Naye Musa akawaambia wana wa Israeli hizo sikukuu za Bwana.