Kutoka
Mlango 16
Kisha wakasafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikilia bara ya Sini, iliyoko kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri.
2 Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung'unikia Musa na Haruni, huko barani;
3 wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote.
4 Ndipo Bwana akamwambia Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo.
5 Kisha itakuwa siku ya sita, ya kwamba watayaandaa hayo watakayoleta ndani, nayo yatakuwa ni mara mbili kuliko wayaokotayo kila siku.
6 Musa na Haruni wakawaambia wana wote wa Israeli, Jioni ndipo mtakapojua ya kuwa Bwana amewaleta kutoka nchi ya Misri;
7 na asubuhi ndipo mtakapouona utukufu wa Bwana; kwa kuwa yeye asikia manung'uniko yenu mliyomnung'unikia Bwana; na sisi tu nani, hata mkatunung'unikia?
8 Musa akasema, Ndilo litakalokuwa, hapo Bwana atakapowapa nyama wakati wa jioni mle, na asubuhi mikate hata mkakinai; kwa kuwa Bwana asikia manung'uniko yenu mliyomnung'unikia yeye; na sisi tu nani? Manung'uniko yenu hayakuwa juu yetu sisi, ila juu ya Bwana.
9 Musa akamwambia Haruni, Haya, sema na mkutano wote wa wana wa Israeli, Njoni karibu mbele ya Bwana; kwa kuwa yeye ameyasikia manung'uniko yenu.
10 Ilikuwa Haruni aliponena na huo mkutano wote wa wana wa Israeli, wakaangalia upande wa bara, na tazama, utukufu wa Bwana ukaonekana katika hilo wingu.
11 Bwana akasema na Musa, akinena,
12 Nimeyasikia manung'uniko ya wana wa Israeli; haya sema nao, ukinena, Wakati wa jioni mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
13 Ikawa wakati wa jioni, kware wakakaribia, wakakifunikiza kituo; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa juu ya nchi pande zote za kituo.
14 Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi.
15 Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao Bwana amewapa ninyi, mle.
16 Neno hili ndilo aliloagiza Bwana, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi, kama hesabu ya watu wenu ilivyo; ndivyo mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake.
17 Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua.
18 Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa.
19 Musa akawaambia, Mtu awaye yote asikisaze hata asubuhi.
20 Lakini hawakumsikiza Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana.
21 Basi wakaokota asubuhi baada ya asubuhi, kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa; na hapo jua lilipokuwa ni kali, kikayeyuka.
22 Basi ikawa siku ya sita wakaokota kile chakula sehemu maradufu, kila mtu pishi mbili; na wazee wote wa mkutano wakaenda na kumwambia Musa.
23 Akawaambia, Ndilo neno alilonena Bwana Kesho ni starehe takatifu, Sabato takatifu kwa Bwana; okeni mtakachooka, na kutokosa mtakachotokosa; na hicho kitakachowasalia jiwekeeni kilindwe hata asubuhi.
24 Basi wakakiweka hata asubuhi, kama Musa alivyowaagiza; nacho hakikutoa uvundo wala kuingia mabuu.
25 Musa akasema, Haya, kuleni hiki leo; kwa kuwa leo ni Sabato ya Bwana; leo hamtakiona nje barani.
26 Siku sita mtaokota; lakini siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana.
27 Ikawa siku ya saba wengine wakatoka kwenda kukiokota, wasikione.
28 Bwana akamwambia Musa, Mtakataa kuyashika maagizo yangu na sheria zangu hata lini?
29 Angalieni, kwa kuwa Bwana amewapa ninyi hiyo Sabato, kwa sababu hii huwapa siku ya sita chakula cha siku mbili; kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote asiondoke mahali pake kwa siku ya saba.
30 Basi hao watu wakapumzika kwa siku ya saba.
31 Na nyumba ya Israeli wakakiita jina lake Mana; nacho kilikuwa mfano wa chembe za mtama, nyeupe; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya maandazi membamba yaliyoandaliwa kwa asali.
32 Musa akasema, Hili ni neno Bwana aliloliamuru, Pishi moja ya kitu hicho na kiwekwe kwa ajili ya vizazi vyenu; ili kwamba wao wapate kukiona kile chakula nilichowalisha ninyi barani, hapo nilipowaleta kutoka nchi ya Misri.
33 Basi Musa akamwambia Haruni, Twaa kopo, ukatie pishi moja ya hiyo Mana ndani yake, uiweke mbele ya Bwana, ilindwe kwa ajili ya vizazi vyenu.
34 Kama vile Bwana alivyomwagizia Musa ndivyo Haruni alivyoiweka hapo mbele ya Ushahidi, ili ilindwe.
35 Na wana wa Israeli walikula Mana muda wa miaka arobaini, hata walipofikilia nchi iliyo na watu, wakala ile Mana, hata walipofikilia mipakani mwa nchi ya Kanaani.
36 Hiyo omeri ni sehemu kumi ya efa.