Waefeso

1 2 3 4 5 6

0:00
0:00

Mlango 4

Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa;
2 kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo;
3 na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.
4 Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.
5 Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.
6 Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.
7 Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo.
8 Hivyo husema, Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa.
9 Basi neno hilo, Alipaa, maana yake nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini za nchi?
10 Naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote.
11 Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;
12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;
13 hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;
14 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.
15 Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.
16 Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo.
17 Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao;
18 ambao; akili zao zimetiwa giza, nao wamefarikishwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao;
19 ambao wakiisha kufa ganzi wanajitia katika mambo ya ufisadi wapate kufanyiza kila namna ya uchafu kwa kutamani.
20 Bali ninyi, sivyo mlivyojifunza Kristo;
21 ikiwa mlimsikia mkafundishwa katika yeye, kama kweli ilivyo katika Yesu,
22 mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya;
23 na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu;
24 mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.
25 Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake.
26 Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka;
27 wala msimpe Ibilisi nafasi.
28 Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji.
29 Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.
30 Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.
31 Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya;
32 tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.