Wagalatia
Mlango 4
Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote;
2 bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba.
3 Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia.
4 Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,
5 kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.
6 Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.
7 Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.
8 Lakini wakati ule, kwa kuwa hamkumjua Mungu, mliwatumikia wao ambao kwa asili si miungu.
9 Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena?
10 Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka.
11 Nawachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu.
12 Ndugu zangu, nawasihi, iweni kama mimi, maana mimi ni kama ninyi. Hamkunidhulumu kwa lo lote.
13 Lakini mwajua ya kuwa naliwahubiri Injili mara ya kwanza kwa sababu ya udhaifu wa mwili;
14 na jaribu lililowapata katika mwili wangu hamkulidharau wala kulikataa, bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu.
15 Ku wapi, basi, kule kujiita heri? Maana nawashuhudu kwamba, kama ingaliwezekana, mngaling'oa macho yenu, mkanipa mimi.
16 Je! Nimekuwa adui wenu kwa sababu nawaambia yaliyo kweli?
17 Hao wana shauku nanyi, lakini si kwa njia nzuri, bali wanataka kuwafungia nje, ili kwamba ninyi mwaonee wao shauku.
18 Navyo ni vizuri kuonewa shauku katika neno jema sikuzote, wala si wakati nikiwapo mimi pamoja nanyi tu.
19 Vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu;
20 laiti ningekuwapo pamoja nanyi sasa, na kuigeuza sauti yangu! Maana naona shaka kwa ajili yenu.
21 Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je! Hamwisikii sheria?
22 Kwa maana imeandikwa ya kuwa, Ibrahimu alikuwa na wana wawili mmoja kwa mjakazi, na mmoja kwa mwungwana.
23 Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi.
24 Mambo haya husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, moja kutoka mlima Sinai, lizaalo kwa utumwa, ambalo ni Hajiri.
25 Maana Hajiri ni kama mlima Sinai ulioko Arabuni, umelingana na Yerusalemu wa sasa; kwa kuwa anatumika pamoja na watoto.
26 Bali Yerusalemu wa juu ni mwungwana, naye ndiye mama yetu sisi.
27 Kwa maana imeandikwa, Furahi, wewe uliye tasa, usiyezaa; Paza sauti, ulie, wewe usiye na utungu; Maana watoto wake aliyeachwa pekee ni wengi Kuliko wa huyo aliye na mume.
28 Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi.
29 Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa.
30 Lakini lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa mwungwana.
31 Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye mwungwana.