0:00
0:00

Mlango 13

Katika siku hiyo watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, watafunguliwa chemchemi kwa dhambi na kwa unajisi.
2 Kisha itakuwa katika siku hiyo, asema Bwana wa majeshi, nitakatilia mbali majina ya sanamu katika nchi, yasikumbukwe tena; pia nitawafukuza manabii, na roho ya uchafu, watoke katika nchi.
3 Tena itakuwa ya kwamba, mtu awaye yote atakapotoa unabii, basi baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, Hutaishi; kwa maana unanena maneno ya uongo kwa jina la Bwana; na baba yake na mama yake waliomzaa watamtumbua atoapo unabii.
4 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba manabii, kila mmoja wao, atayaonea haya maono yake atoapo unabii; wala hawatavaa joho ya nywele ili kudanganya watu;
5 bali atasema, Mimi si nabii kamwe; mimi ni mkulima wa nchi; kwa maana nalifanywa mtumwa tokea ujana wangu.
6 Na mtu atamwambia, Je! Jeraha hizi ulizo nazo kati ya mikono yako ni nini? Naye atajibu, Ni jeraha nilizotiwa katika nyumba ya rafiki zangu.
7 Amka, Ee upanga, juu ya mchungaji wangu, na juu ya mtu aliye mwenzangu, asema Bwana wa majeshi; mpige mchungaji, nao kondoo watatawanyika; nami nitaugeuza mkono wangu juu ya wadogo.
8 Hata itakuwa, ya kwamba katika nchi yote mafungu mawili yatakatiliwa mbali, nao watakufa, asema Bwana; lakini fungu la tatu litabaki humo.
9 Nami nitalileta fungu lile la tatu na kulipitisha kati ya moto, nami nitawasafisha kama fedha isafishwavyo, nami nitawajaribu kama dhahabu ijaribiwavyo; wataliitia jina langu, nami nitawasikia; mimi nitasema, Watu hawa ndio wangu; nao watasema, Bwana ndiye Mungu wangu.